Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
Ujumbe wa Kamishna wa Bima wafika Kanda ya Pemba; Utambuzi wa usajili wa watoa huduma za afya waendelea
27 Nov, 2025
Ujumbe wa Kamishna wa Bima wafika  Kanda ya Pemba; Utambuzi wa usajili wa watoa huduma za afya waendelea

Ujumbe wa Watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ukiongozwa na Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo Saqware pamoja na Naibu Kamishna Bi. Khadija Said umetembelea Kanda ya Pemba leo Novemba 26, 2025 na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Kanda hiyo ikiwemo maendeleo ya Usajili wa watoa huduma za afya.
Akitoa maelezo ya utangulizi Dkt. Saqware amesema ziara hiyo ni mfululizo wa utekelezaji wa kazi za Mamlaka ambapo kwa kipindi cha ndani ya mwezi mmoja ameshatembelea Kanda 8 ambapo amekuwa akipata fursa ya kujionea utendaji kazi wa kanda hizo hususan kwenye eneo la usimamizi wa skimu za bima ya afya sambamba na kubaini changamoto mbalimbali zinazozikabili Kanda hizo na kuweka mikakati thabiti ya kukabiliana na changamoto hizo.
Akiwasilisha utekelezaji wa majukumu ya Kanda hiyo ya Pemba Meneja Sharifu Hamadi amesema Kanda hiyo inaendelea kufanya juhudi za kuwatambua na kuwasajili watoa huduma za Afya (HSPs) wanaohudumia wanachama na wanufaika wa Skimu za bima ya afya ambapo wametembelea vituo hivyo na kuonana na Uongozi wa vituo na kutoa elimu.
Kanda ya Pemba inasimamia mikoa miwili, mkoa wa Kusini Pemba ambao una wilaya ya Chake chake na Mkoani, na Mkoa wa Kaskazini Pemba ambao una wilaya ya Wete na Micheweni. Kisiwa cha Pemba kina eneo la kilomita za mraba 988 na kina idadi ya watu wanaokisiwa kufikia 606,022
 
TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA