Kamishna wa bima awataka wadau wa bima kuhudumia wananchi kwa uweledi.
Kamishna wa Bima nchini Dkt. Baghayo Saqware amewataka wadau wa sekta ya bima nchini kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi wanaowahudumia. Hayo ameyasema katika kikao chake cha kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi na wadau wa bima wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini jijini Mbeya.
“Mamlaka ya bima iliundwa na serikali kutetea haki za wateja kwa kukagua, kusimamia uhai, uhimilivu na uweledi. Fedha za soko la bima ni fedha za watanzania ambazo ni muhimu kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Hivyo, ni muhimu zilindwe kwa umakini mkubwa” alisema Dkt Saqware.
Pia amesema kuwa biashara ya bima ni biashara ya muda mrefu ambayo kwa namna yeyote kampuni itakayosajiliwa nchini itapaswa kuhudumia wananchi, hivyo si rahisi kwa kampuni kufungwa bila kujali maslahi ya mapana ya wananchi.
“Leo nimekuja hapa ili tupate fursa ya kuainisha maeneo mbalimbali yanayosababnisha wananchi wasipate haki zao kutoka kwa kampuni za bima tulizozisajili kwani serikali imekasimu wajibu kwetu ili tuweze kuendeleza soko la bima na kutoa fidia kwa wananchi” aliongeza Dkt. Saqware.
Kamishna amewataka wadau wote waliopata leseni watambue kuwa wana kazi ya kuendeleza na kusimamia majukumu ya Mamlaka kama walivyokasimiwa kupitia sheria ya bima. Kwani kwa yeyote aliyepewa leseni kutoka Mamlaka atakuwa amekasimiwa kutekeleza kazi za Mamlaka kwa kuhudumia umma kwa uweledi.
“Tunapokea maoni ya kuboresha utendaji wa Mamlaka na kuendeleza soko la bima kwa kuhakikisha sekta ya bima nchini inakuwa mchango mkubwa kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” alisisitiza Dkt. Saqware.
Mamlaka katika mwaka wa biashara 2023 imepanga kuhakikisha kuna ongeza la wigo wa usambazaji na upatikaki huduma za bima nchini, kuongeza watumiaji bima mbalimbali ikiwe za kilimo, maisha, uvuvi na kuwafikia wafanyabiashara wadogo. Pia, kutekeleza mpango wa serikali wa kuendeleza soko la bima nchini.
Afisa Tehama wa Mamlaka Bw. Seif Bakari akitoa mada kuhusu mifumo ya usimamizi ya soko la bima nchini katika kikao cha kusikiliza malalamiko ya huduma za bima kutoka Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Naibu Kamishna wa Bima Bi. Khadija Issa Said akitoa neno la ufunguzi katika kikao cha kusikiliza malalamiko ya huduma za bima kutoka Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Sehemu ya wananchi waliyohudhuria katika kikao cha kusikiliza malalamiko ya huduma za bima kutoka Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo Saqware aongea na wadau wa bima katika kikao cha kusikiliza malalamiko ya huduma za bima kutoka Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.