Wajumbe Bodi ya Taifa ya Bima wanolewa mada mbalimbali kuhusu bima

Mafunzo kwa Wajumbe wa Bodi ya Taifa ya Bima (NIB) yamefanyika leo katika ukumbi wa mikutano ZURA, Zanzibar. Lengo ma mafunzo hayo ni kueleza shughuli mbalimbali za Mamlaka kwa wajumbe wa Bodi hiyo ili kuongeza uelewa na kupata maoni kuhusu sekta hiyo, mafunzo hayo yamehudhuriwa pia na viongozi wakuu wa Mamlaka, Menejimenti na baadhi ya watumishi wa taasisi hiyo.
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ndio mratibu wa mafunzo hayo ambapo mada zilizowasilishwa ni pamoja na Skimu ya bima ya kilimo, Bima ya Afya kwa Wote na masuala ya Hatifungani (bonds). Katika wasilisho la bima ya afya na kilimo lilizingatia namna ya utekelezaji wake, sheria zinazosimamia, kulindwa kwa walaji na masuala mengine muhimu.
Akifungua rasmi Mafunzo hayo Makamu Mwenyekiti wa Bodi Dkt. Suleiman Mohamed kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi hiyo CPA Moremi Marwa amesema “Kupitia mafunzo haya tunapata fursa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu maendeleo na utatuzi wa changamoto katika sekta ya bima”
Aidha Kamishna wa Bima Tanzania Dkt. Baghayo Saqware amesema “Ni matarajio yetu mafunzo haya yametoa uelewa mpana kwa wajumbe wa Bodi kuhusu utekelezaji wa mikakati na mipango ya Mamlaka hasa katika maeneo muhimu yanayogusa maisha ya watanzania wengi, tunaithamini michango yenu kwa maendeleo ya taasisi yetu na sekta hii”
Pia mjumbe kutoka Bodi hiyo, Bi. Emmy Hudson ameshukuru Mamlaka kwa kuwapatia mafunzo hayo akisisitiza kama wajumbe wana kazi ya kushauri Mamlaka ili iweze kufikia Malengo iliyojiwekea kukuza sekta ya bima hivyo mafunzo hayo yameongeza uelewa.
TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA