Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
Wadau wa Bima Wajadili Njia Bora kufikisha huduma kwa Wananchi
03 Oct, 2022
Wadau wa Bima Wajadili Njia Bora kufikisha huduma kwa Wananchi

Wadau wa bima nchini wamefanya kongamano la kujadili njia bora zaidi za kupeleka huduma za bima kwa Wananchi hasa wanaoishi vijijini.

Kongamano hilo lililoandaliwa na Chuo cha Bima na Hifadhi ya Jamii Afrika (ACISP) limefanyika Hoteli ya Four Points Jijini Dar es Salaam ambapo wataalamu wa Bima na watoa huduma za bima nchini waliwasilisha mada mbalimbali na kujadili kwa kina njia stahiki za kusambaza huduma za bima.

Akitoa mada katika kongamano hilo kuhusu wajibu na hatua zinazochukuliwa na Mamlaka ili kuboresha huduma za bima kwa Wananchi, Kamishna wa Bima Nchini Dkt. Baghayo Saqware alisema TIRA iko mstari wa mbele kuhakikisha njia za  usambazaji wa bima zinapata baraka za Mamlaka ikiwa ni pamoja na kufuata miongozo stahiki. “Hivi karibuni Mamlaka imetoa miongozo kuhusu mifumo ya kidigitali ili itumike katika kusambaza Bima kwa Wananchi” alisema Dkt. Saqware.

Akifafanua ufikiwaji wa huduma ya bima nchini, Dkt. Saqware alisema “kwa sasa watu wazima Watanzania wanaotumia bima ya aina moja au nyingine iwe mali, afya au maisha ni asilimia 16 tu na matarajio yetu ni kufikia asilimia 50 ya watu wazima nchini miaka kumi ijayo”.

Kwa upande wake Mwenyekiti Mtendaji wa ACISP Bw. Sosthenes Kewe alisema kongamano hilo lilijikita katika kutafuta njia mbadala za usambazaji wa huduma za bima tofauti na njia tulizozizoea. Bw. Kewe alisema kusambaza huduma za bima ni muhimu sana katika kujenga ustahimilivu na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi na kwa bei nafuu.