Viongozi wa wilaya ya Ilemela wapata elimu ya bima ya afya kwa wote
VIONGOZI WA WILAYA YA ILEMELA WAPATA ELIMU YA BIMA YA AFYA KWA WOTE
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Kanda ya Ziwa imetoa elimu kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote kwa Viongozi wa Wilaya ya Ilemela, ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za afya kwa usawa na kwa gharama nafuu.
Elimu hiyo imelenga kuwawezesha viongozi hao kuelewa wajibu wao katika kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo ngazi ya serikali za mitaa na kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika mfumo ya bima ya afya kwa wote. Viongozi hao ni Kamati ya Usalama ya Wilaya, Mbunge, Madiwani, Watendaji wa kata, mitaa na vijiji, Wenyeviti wa mitaa na vijiji wotw wa wilaya ya Ilemela.
Akizungumza katika kikao hicho, Meneja wa TIRA Kanda ya Ziwa, Bw. Oyuke Phostine, amesema Mamlaka ipo tayari kusimamia utekelezaji wa Sheria hiyo pamoja na kanuni zake katika maeneo yote yaliyo chini ya usimamizi na udhibiti wa TIRA. Ameeleza kuwa TIRA itahakikisha skimu zote za bima ya afya zinafuata sheria, misingi ya haki kwa wanachama na viwango vilivyowekwa ili kulinda maslahi ya wananchi.
Bw. Oyuke ameongeza kuwa TIRA itaendelea na jukumu la kutunza na kuhuisha kanzidata ya Vituo vya Kutolea Huduma za Afya vilivyoidhinishwa, ili kuhakikisha vituo hivyo vinatoa huduma bora, salama na zenye viwango vinavyokubalika na kupata taarifa sahihi za vituo vinavyotoa huduma chini ya skimu mbalimbali za bima ya afya, hivyo kuongeza uwazi na ufanisi katika utoaji wa huduma.
Aidha, Mamlaka itaendelea na ukukaguzi wa mara kwa mara wa Skimu za Bima ya Afya ili kuhakikisha zinazingatia matakwa ya sheria na kutoa huduma stahiki kwa wanachama wake kwa lengo la kufanikisha azma ya taifa ya kufikia bima ya afya kwa wote.
