Viongozi kutoka Eswatini wazuru TIRA kupata uzoefu wa masuala ya kibima

Aprili 8, 2025 Ujumbe wa watu 12 kutoka Eswatini ukiongozwa na Naibu Spika wa Bunge la Nchi hiyo Mhe. Madala Mhlanga umezuru ofisi ndogo za makao makuu ya TIRA Dar es salaam kwa lengo la kupata uzoefu wa masuala mbambali ya kibima ikiwemo yahusuyo Usimamizi wa Soko na maswala ya sheria.
Baadhi ya wageni hao pia wanatoka katika Bunge la Nchi hiyo, Wizara ya Fedha na Mamlaka ya masuala ya huduma za Fedha zisizo za kibenki nchini humo (Financial Services Regulatory Authority), ambapo waliungana na wataalamu wengine kutoka TIRA na kufanya kikao chenye lengo la kupeana uzoefu wa namna ya usimamizi na udhibiti katika soko la bima kwa pande zote mbili.
Aidha, kikao hicho kiliongozwa na Mkurugenzi wa Usimamizi kutoka Mamlaka Bw. Christopher Mapunda kwa niaba ya Kamishna wa Bima Tanzania ambapo wageni hao walipitishwa katika mada iliyoelezea hali ya soko la bima nchini ikijumuisha usimamizi wa soko la bima, sheria zinazotumika kusimamia soko la bima, Mamlaka ya Kamishna kwenye kusimamia soko la bima na mifumo ya tehama.
Aidha mjadala pia ulijikita kwenye kwenye vipaumbele mbalimbali vya Mamlaka vikiwemo Utekelezwaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote (UHI) na Uanzishwaji wa konsotia ya bima ya kilimo (TAIC).
Awali Naibu Spika wa Nchi hiyo Mhe. Madala alieleza wapo katika mchakato wa uboreshaji wa sheria ya nchini humo na hivyo wamechagua Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazofanya vizuri katika masuala ya bima ili kuweza kujifunza. Zaidi ameishukuru Mamlaka kwa elimu na uzoefu waliopata huku wakiahidi kuendeleza ushirikiano kwa siku zijazo.
TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA