Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
“Tumeboresha Mifumo ya Kidigitali Sekta ya Bima” – Dkt. Baghayo Saqware aeleza Mafanikio Sita ya Sekta kwa Mwaka 2024
17 Oct, 2025
“Tumeboresha Mifumo ya Kidigitali Sekta ya Bima” – Dkt. Baghayo Saqware aeleza Mafanikio Sita ya Sekta kwa Mwaka 2024

Dodoma, 16 Oktoba 2025 — Kamishna wa Bima, Dkt. Baghayo Saqware, amesema sekta ya bima nchini imepiga hatua kubwa katika mwaka 2024, hususan kupitia maboresho ya mifumo ya kidigitali yanayolenga kuongeza ufanisi na uwazi katika usimamizi wa sekta hiyo. Akizungumza katika uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa Soko la Bima kwa Mwaka 2024, uliofanyika katika jengo jipya la TIRA Bima House jijini Dodoma, Dkt. Saqware alisema:
“Tumeboresha mifumo ya kidigitali sekta ya bima ili kuongeza usambazaji na uandikishaji wa bima kwa haraka, ufanisi na uwazi. Lengo letu ni kuhakikisha huduma za bima zinapatikana kwa urahisi zaidi kwa Watanzania wote.”

Dkt. Saqware alitaja mafanikio sita yaliyopatikana katika sekta ya bima mwaka 2024, ikiwemo kuboresha mifumo ya kidigitali, utekelezaji wa Bima ya Safari kwa Wageni (Inbound Mandatory Travelling Insurance) Zanzibar, usimamizi wa utekelezaji wa Sheria na Kanuni za Bima ya Afya kwa Wote, uimarishaji wa usimamizi wa bima za lazima, utoaji wa miongozo mbalimbali ya sekta, pamoja na uanzishwaji wa konsotia mbili muhimu – ya Kilimo na ya Mafuta na Gesi.

Akizungumzia matarajio ya TIRA kwa miaka ijayo, Kamishna alisema Mamlaka inalenga kuendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa njia ya kidigitali, kuongeza wigo wa bima jumuishi kufikia asilimia 3 ifikapo mwaka 2030, na kuongeza wastani wa watumiaji wa bima kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2050. Pia alieleza kuwa TIRA inaendelea na juhudi za marekebisho ya Sheria ya Bima, kutengeneza Sera ya Taifa ya Bima, na kuimarisha mikakati ya utoaji wa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa bima.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Bima ya Taifa, CPA Moremi Marwa, aliipongeza TIRA kwa mafanikio hayo na kueleza kuwa Bodi itaendelea kushirikiana na Mamlaka kutoa miongozo na maelekezo kulingana na sera na sheria zilizopo. Alisisitiza umuhimu wa uadilifu, ubora na uwazi katika utoaji wa huduma za bima, akisema hayo ndiyo misingi ya kuijenga sekta yenye uaminifu na uendelevu.

TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA