TIRA yazindua rasmi Jengo Jipya la Makao Makuu – “TIRA Bima House” Dodoma

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) leo tarehe 16 Oktoba 2025 imezindua rasmi Jengo jipya la Makao Makuu yake lililopo Njedengwa, Dodoma, linalojulikana kama TIRA Bima House. Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, wadau wa sekta ya bima, na wawakilishi wa taasisi za fedha. Tukio hilo limekuwa alama muhimu katika historia ya TIRA, likionesha hatua kubwa ya maendeleo katika kuboresha mazingira ya kazi na kuimarisha usimamizi wa sekta ya bima nchini.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Sera na Mipango Zanzibar, Mhe. Saada Mkuya Salum, ambaye alilipongeza TIRA kwa hatua hiyo ya kihistoria na kusisitiza kuwa ujenzi wa jengo hilo ni kielelezo cha utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuhamishia taasisi zake zote Dodoma na kuimarisha utendaji unaoendana na maendeleo ya uchumi wa kisasa. Alibainisha kuwa TIRA imeendelea kuwa chachu katika kukuza sekta ya bima nchini, na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kuhakikisha sekta hiyo inachangia ipasavyo katika pato la taifa na ustawi wa wananchi.
Katika hotuba yake, Mhe. Mkuya aliitaka TIRA kuendelea na juhudi za kusimamia kwa weledi utekelezaji wa Sheria ya Bima, kuhakikisha kuwa watoa huduma wa bima wanazingatia kanuni na viwango vilivyowekwa, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya faida za bima. Aidha, alihimiza sekta ya bima kuwekeza zaidi katika ubunifu wa bidhaa zinazokidhi mahitaji ya Watanzania, hasa katika maeneo ya kilimo, afya, na majanga ya asili.
Kwa upande wake, Kamishna wa Bima, Dkt. Baghayo Saqware, alieleza kuwa uzinduzi wa TIRA Bima House ni hatua muhimu kuelekea utoaji bora wa huduma, uwazi, na uwajibikaji katika kusimamia sekta ya bima. Alisema jengo hilo jipya litakuwa kitovu cha ubunifu na usimamizi wa sekta, na kuahidi kwamba TIRA itaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na wadau wote wa bima ili kujenga sekta imara, jumuishi na endelevu kwa maendeleo ya taifa.
TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA