TIRA yaweka mkazo Utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote – Mafunzo yafanyika Iringa
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), kupitia Ofisi ya Kanda ya Kati, imetoa elimu kuhusu masuala muhimu ya bima, ikiwemo elimu juu ya utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, Sura ya 161. Elimu hiyo ilitolewa tarehe 24 Oktoba 2025 kwa Waganga Wafawidhi wa Wilaya kutoka katika Halmashauri ya Iringa.
Aidha, lengo kuu la mafunzo hayo lilikuwa ni kuongeza uelewa kuhusu utekelezaji wa sheria hiyo, inayolenga kuhakikisha watanzania wote wanapata huduma bora, nafuu na endelevu za afya kupitia mfumo wa bima. Kupitia mafunzo hayo, washiriki walijengewa uwezo wa kuelewa majukumu yao katika kufanikisha utekelezaji wa sheria hiyo ndani ya vituo vyao vya kutolea huduma za afya.
Kikao hicho pia kilihusisha takribani vituo vya afya 100 vilivyopo chini ya Halmashauri ya Iringa, ambapo washiriki walipata nafasi ya kujadili kwa kina namna bora ya kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya afya na sekta ya bima. Aidha, vituo zaidi ya 180 vimeshasajiliwa rasmi na kutambuliwa na TIRA kwa ajili ya kutoa huduma chini ya mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.
Kupitia kampeni endelevu za utoaji elimu, TIRA Kanda ya Kati inaendelea kushirikiana na taasisi za umma na binafsi katika kuhamasisha uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa bima kama nyenzo ya msingi katika kuboresha ustawi wa wananchi, kuongeza usalama wa kifedha, na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA
