TIRA yawanoa Mawakili wa Serikali Sheria, Taratibu na Kanuni za Bima zaelezwa

Katika kuhakikisha Sheria, Taratibu, Kanuni na Miongozo ya Bima inafuatwa, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imetoa semina ya masuala ya bima kwa Mawakili wa Serikali nchini ili kuwaongezea uelewa katika kutekeleza majukumu yao. Semina hiyo ilifanyika katika ukumbi wa Vizano Hotel, Octoba 10, 2025 jijini Dodoma.
Akifungua Mkutano huo Mkurugenzi Msaidizi Uratibu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Ipyana Mlilo kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali; aliipongeza TIRA kwa kuandaa mafunzo hayo yaliyolenga kujenga uwezo wa kisheria na kitaalamu kwa Mawakili yakisimamia Utekelezaji wa Malengo ya Dira 2050 na pia alitoa rai kwa Taasisi nyingine kuiga mfano wa Mamlaka kwa kutoa mafunzo kama hayo.
Kwa upande wa Mamlaka; Bi. Margaret Mngumi, Msuluhishi wa Migogoro ya Bima kwa niaba ya Kamishna wa Bima alisema TIRA itaendelea kutoa Mafunzo yahusuyo bima ili kuhakikisha wanasheria wa Serikali na wadau wengine wanaongeza uelewa wa masuala ya bima. Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria TIRA; Bw. Ponziano Lukosi alisema bima ni hitaji la msingi kwa kila Mwananchi na kusisitiza kuwa ni sekta ya muhimu sana hivyo mafunzo hayo yatasaidia Mawakili waweze kutoa msaada stahiki na kwa wakati kwa wananchi.
Aidha, Mawasilisho Matano yenye mada mbalimbali zikiwemo Sheria za Bima ya afya kwa wote, Uhusiano wa Mawakili wa Serikali na sekta ya bima, Sheria za Bima, Majukumu ya Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima Tanzania (TIO) yaliwasilishwa. Mada hizo zilitoa fursa ya maswali na majibu kuhusu masuala hayo ya bima lakini pia yaliongeza uhusiano imara kati ya TIRA na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa maendeleo ya taifa letu.
TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA