Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
TIRA na wadau wa Bima watoa msaada shule ya Sekondari Jangwani
23 Sep, 2025
TIRA na wadau wa Bima watoa msaada shule ya Sekondari Jangwani

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imeonyesha mshikamano wake na juhudi za kuinua kiwango cha elimu nchini kwa kutoa msaada wa vifaa muhimu vya kujifunzia katika Shule ya Sekondari Jangwani, jijini Dar es Salaam. Katika tukio lililofanyika shuleni hapo tarehe 22 Septemba 2025, TIRA kwa kushirikiana na Wadau wake yaani Kampuni za Bima inazozisimamia ilikabidhi viti 200 na meza 200 kwa wanafunzi, pamoja na viti 32 na meza 32 vya kisasa kwa walimu, kama sehemu ya mchango wake katika kuimarisha mazingira ya kujifunzia. Kampuni zilizochangia ni TAN-RE, GRAND-RE na MO 

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Kamishna wa Bima, Dkt. Baghayo Saqware, alieleza kuwa msaada huo ni sehemu ya mpango wa taasisi hiyo na Kampuni za Bima wa kurudisha kwa jamii kupitia shughuli za kijamii (CSR). Alinukuliwa akisema; “mazingira bora ya kujifunzia ni nguzo muhimu ya mafanikio ya kitaaluma kwa wanafunzi, na kuongeza kuwa TIRA itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu kuhakikisha elimu bora inapatikana kwa wote”. Alisema Dkt. Saqware.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Jangwani aliishukuru Mamlaka (TIRA) kwa mchango huo, akieleza kuwa vifaa hivyo vitasaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa samani darasani, jambo ambalo lilikuwa likikwamisha maendeleo ya wanafunzi. Alisema kuwa shule hiyo ina idadi kubwa ya wanafunzi, na msaada huo utasaidia kuongeza ufanisi wa ufundishaji na ujifunzaji.

Wanafunzi nao walionesha furaha yao kupitia ujumbe mfupi wa shukrani uliotolewa na dada Mkuu wa Shule Bi. Neema Evance  Kidato cha 6 CBN,  akisema kuwa msaada huo umewatia moyo na kuwapa hamasa ya kusoma kwa bidii zaidi. Walieleza kuwa uwepo wa madawati na viti vya kutosha utapunguza msongamano na pilika pilika za kunyang’anyana viti na kuwapa nafasi nzuri ya kujifunza kwa utulivu hasa kwa wanafunzi wenye uhitaji maalum.

Hatua hii ya TIRA ni mfano wa kuigwa kwa taasisi nyingine nchini, hasa zile zinazofaidika na rasilimali za taifa, kuchangia katika kuinua sekta ya elimu. Uwekezaji katika elimu ni uwekezaji wa baadaye, na msaada huu wa TIRA ni ushahidi wa kujitolea kwao katika maendeleo ya taifa.

Kwa ujumla, msaada huo wa TIRA umepokelewa kwa mikono miwili na unatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika ubora wa elimu Jangwani Sekondari, ikiwa ni hatua moja muhimu kuelekea katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya elimu nchini kama inavyosisitizwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA