TIRA yatoa Semina ya Elimu ya Sheria ya Bima kwa Mahakimu Mkoa wa Singida

Tarehe 26, Septemba 2025 – Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) – Kanda ya Magharibi iliendesha semina ya elimu ya Sheria ya Bima kwa Mahakimu Wakazi wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya za Mkoa wa Singida. Semina hiyo ilifanyika katika ukumbi wa Jmax, Wilaya ya Manyoni.
Aidha, Lengo kuu la semina hiyo lilikuwa kuwajengea Mahakimu uelewa mpana kuhusu masuala ya bima, ili kuongeza ufanisi katika kushughulikia mashauri yanayohusiana na sekta ya bima. Kupitia semina hii, TIRA inalenga kuimarisha ushirikiano na mhimili wa Mahakama, kuhakikisha kuwa utekelezaji wa sheria za bima unafanyika kwa ufanisi, uwazi na kwa manufaa ya wananchi.
Akizungumza wakati wa kufunga semina hiyo, Meneja wa Kanda ya Magharibi Bi Awanje Matenda alisisitiza dhamira ya TIRA kuendelea kutoa elimu na kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya bima ili kuhakikisha kuwa haki na wajibu wa wadau wote wa bima unazingatiwa na kulindwa ipasavyo.
Semina hiyo pia iliwahusisha Wanasheria kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa bima ambao walito somo kuhusu Sheria hizo kufatwa katika utekelezaji wa majukumu yao. Mamlaka itaendelea kutoa elimu kwa wadau wa sekta ya bima na umma kwa ujumla kwa lengo la kuongeza uelewa wa masuala ya bima na kuchochea ukuaji wa sekta ya bima nchini.
TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA.