TIRA yashiriki zoezi la kujengea uwezo viongozi na wadau wa afya mkoani Shinyanga
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kupitia Kanda ya Magharibi; imeshiriki katika zoezi la kujengea uwezo viongozi na wadau wa sekta ya afya mkoani Shinyanga ikiwa na lengo la kueleza jukumu la Mamlaka katika Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote. Mkutano huo umefanyika tarehe 17 Desemba, 2025.
Zoezi hilo lilihusisha viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Shinyanga akiwemo Mkuu wa Mkoa (RC), Katibu Tawala wa Mkoa (RAS), Maafisa Afya wa Mkoa (RMOs), Maafisa Afya wa Wilaya (DMOs), pamoja na watoa huduma za afya kutoka Shinyanga Mjini na wadau wa Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote (UHI).
Katika zoezi hilo, TIRA pia ilipata fursa ya kuwasilisha tuzo ya kutambua mchango maalum kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, CP Salum Rashid Hamduni, kwa mchango wake mkubwa katika kuwezesha usajili wa vituo vingi vya huduma za afya mkoani humo.
Tuzo hiyo ilikabidhiwa na Meneja wa TIRA Kanda ya Magharibi Bi. Awanje Matenda kwa niaba ya Kamishna wa Bima ambaye alimshukuru RAS kwa mchango wake katika sekta ya bima pamoja na wadau wengine waliohudhuria mkutano huo. TIRA ina jukumu kuu la usimamizi katika mpango wa bima ya afya kwa wote.
TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA
