TIRA yashiriki Mkutano Mkuu wa CISNA 2025; Majadiliano mbalimbali kukuza sekta ya bima yafanyika

TIRA yashiriki Mkutano Mkuu wa CISNA 2025; Majadiliano mbalimbali kukuza sekta ya bima yafanyika
Mkutano Mkuu wa 48 wa Kamati ya Mamlaka ya Bima, Masoko ya Mitaji na Taasisi zisizo za Kibenki (CISNA) ambayo ni kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) unaendelea mjini Maun, Botswana, kuanzia tarehe 5 hadi 10 Oktoba 2025, ambapo Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) inashiriki.
TIRA ni mwanachama wa CISNA kutokana na wajibu wake wa kusimamia sekta ndogo ya bima nchini. Mkutano huu unajumuisha vikao kazi vya kamati ndogo tatu — Capital Markets (CMS), Insurance and Retirement Funds, Medical Schemes and Intermediaries (IRMIS), na Microfinance and Financial Co-operatives (MiFFCO) — pamoja na kikao cha Governance Council na Baraza Kuu la CISNA (General Council Meeting).
Moja ya jukumu la CISNA ni Kuoanisha mifumo ya udhibiti na kukuza utekelezaji wa viwango vya kimataifa vya huduma za kifedha zisizo za kibenki.CISNA inalenga kuhakikisha kwamba Mamlaka zote za udhibiti wa sekta za bima, masoko ya mitaji (securities), na taasisi zisizo za kibenki katika nchi wanachama wa SADC zinafanya kazi kwa viwango vinavyolingana na vinavyoendana na viwango vya kimataifa.
Aidha, kikao hicho kilifunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Botswana mnamo tarehe 7 Oktoba 2025, kikihudhuriwa na wajumbe kutoka nchi wanachama wa SADC na wawakilishi wa taasisi za kikanda kama SADC Secretariat, ESAAMLG, CCBG, DFRC, na CoSSE. Miongoni mwa masuala yanayojadiliwa ni pamoja na marekebisho ya Kanuni za CISNA (CISNA Rules), ikiwemo pendekezo la nchi mwenyeji wa Sekretarieti kupewa kiti cha kudumu katika Baraza la Uongozi, uidhinishaji wa bajeti na taarifa za fedha, na utekelezaji wa Mkakati wa CISNA 2022–2026.
Tanzania inawakilishwa na Kamishna wa Bima, Dkt. Baghayo A. Saqware, Mkurugenzi wa Mipango, Tafiti na Uendelezaji wa Soko, Bw. Samuel Mwiru, Mkurugenzi wa Leseni na Bima Mtawanyo Bw. Christopher Mapunda na Meneja wa Tathmini Bima na Uthabiti wa fedha Dkt. Peter Tengaa. Ushiriki wa TIRA katika mkutano huu ni sehemu ya jitihada za kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kubadilishana uzoefu wa kiudhibiti, na kukuza ufanisi wa sekta ya bima nchini Tanzania.
TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA