Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
TIRA yashiriki Maonesho ya 8 ya Teknolojia ya Madini Geita, elimu ya bima yatolewa
24 Sep, 2025
TIRA yashiriki Maonesho ya 8 ya Teknolojia ya Madini Geita, elimu ya bima yatolewa

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kupitia Kanda ya Ziwa inashiriki katika Maonesho ya Nane (8) ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea kwenye viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, mkoani Geita kuanzia Septemba 22 – 28, 2025.

Aidha, katika maonesho hayo, kampuni mbalimbali za bima zinashiriki ndani ya banda moja maarufu kama “Kijiji cha Bima”, ambapo zinatoa elimu na huduma za bima kwa wananchi wanaotembelea mabanda hayo pamoja na wafanyabiashara na wafanyakazi wa migodini. Lengo kuu ni kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa bima katika kujikinga dhidi ya ajali na hatari mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika shughuli za kila siku.

Kaimu Meneja wa TIRA Kanda ya Ziwa Bw. Phostine Oyuke alieleza lengo la ushiriki ni kuweka thamani katika mnyororo wa shughuli za madini nchini Tanzania kwa kuelimisha wafanyakazi, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla umuhimu wa kujikinga na bima katika kazi zao mathalani kuwa na bima za afya.

Maonesho ya Teknolojia ya Madini yalianzishwa mwaka 2018 kwa lengo la kuimarisha sekta ya madini nchini na kuhakikisha rasilimali hiyo muhimu inanufaisha Watanzania wote. Yamekuwa jukwaa mahsusi la Serikali, sekta binafsi, wachimbaji wakubwa na wadogo, taasisi za kifedha, wajasiriamali na wadau wa maendeleo kukutana, kujadili na kubadilishana uzoefu.

“Ukuaji wa Sekta ya Madini ni Matokeo ya Matumizi ya Teknolojia Sahihi na Uongozi Bora Shiriki Uchaguzi Mkuu Oktoba, 2025.”

TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA