Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
TIRA Yashiriki Kongamano la Bima ya Afya kwa Wote na Mdahalo wa Kitaifa Kuhusu Ufadhili wa Sekta ya Afya
31 Oct, 2024
TIRA Yashiriki Kongamano la Bima ya Afya kwa Wote na Mdahalo wa Kitaifa Kuhusu Ufadhili wa Sekta ya Afya

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) inashiriki kikamilifu katika Kongamano la Bima ya Afya kwa Wote pamoja na Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Mpango wa Ufadhili wa Sekta ya Afya, yanayofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha, jijini Arusha. Kongamano litafanyika tarehe 29 na 30 Oktoba 2024, likifuatiwa na Mdahalo tarehe 31 Oktoba na 01 Novemba 2024.

Matukio haya makubwa yalipangwa kufunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, tarehe 30 Oktoba 2024, yamewaleta pamoja wataalamu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi. Kongamano hili linalenga kuchambua mikakati bora inayoweza kutumiwa na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuboresha huduma za afya kwa wote.

Malengo makuu ya kongamano ni kujadili ugharamiaji wa huduma za afya na kuweka dira ya utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote nchini Tanzania. Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Ufadhili wa Sekta ya Afya pia unafanyika kama sehemu ya maagizo ya Baraza la Mawaziri wa Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, baada ya kikao chao jijini Dar es Salaam mnamo Mei 2024. Mdahalo huu unatekeleza maazimio ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika yaliyopitishwa jijini Addis Ababa, Ethiopia mnamo Julai 2019.

Mada muhimu zitakazojadiliwa zinajumuisha; Ugharamiaji wa Huduma za Afya kwa Wote: Mikakati bunifu kwa upatikanaji endelevu wa fedha; Nafasi ya Teknolojia na Ubunifu; Kuboresha ufanisi na upatikanaji wa huduma za Bima ya Afya kwa Wote na Mikakati ya Usajili na Usajili Upya: Mbinu zinazofanya kazi na changamoto zake.

Kongamano hili linatarajiwa kuwa na matokeo yenye tija katika kuimarisha mpango wa bima ya afya kwa wote na kuboresha mfumo wa huduma za afya nchini Tanzania na kanda ya Afrika Mashariki kwa ujumla.