Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
TIRA yapanda miti 200 kuunga mkono kampeni ya kijani na kuadhimisha siku ya kuzaliwa; Rais Samia
27 Jan, 2026
TIRA yapanda miti 200 kuunga mkono kampeni ya kijani na kuadhimisha siku ya kuzaliwa; Rais Samia

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) leo asubuhi, tarehe 27 Januari 2026, imepanda miti 200 kuzunguka eneo la Jengo la Njedengwa, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono Kampeni ya Kijani ya kitaifa pamoja na kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Zoezi hilo limeongozwa na Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware, akiambatana na Wakurugenzi na Mameneja wa TIRA pamoja na watumishi wengine. Ushiriki huo umeonesha dhamira ya TIRA katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kulinda mazingira na kuhimiza matumizi endelevu ya rasilimali za asili kwa maendeleo ya taifa.

Akizungumza wakati wa tukio hilo, Dkt. Saqware alisema kuwa upandaji wa miti ni sehemu ya mchango wa TIRA katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, kuboresha mazingira ya kazi na makazi, pamoja na kuhakikisha urithi wa mazingira bora kwa vizazi vijavyo. Alisisitiza kuwa taasisi za umma zina wajibu wa kuwa mfano katika kutekeleza ajenda ya uhifadhi wa mazingira kwa vitendo.

Aidha, Dkt. Saqware alibainisha kuwa kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya Mheshimiwa Rais kwa vitendo kama upandaji miti ni ishara ya kuunga mkono maono yake ya uongozi unaojali mazingira, ustawi wa jamii na maendeleo jumuishi. Alieleza kuwa Kampeni ya Kijani ni moja ya nyenzo muhimu katika kufanikisha ajenda ya Tanzania ya kijani na endelevu.

Katika hatua nyingine, Kamishna wa Bima ameendelea kusisitiza umuhimu wa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, akiwahimiza Watanzania na viongozi katika ngazi zote kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha wananchi kujiunga na mfumo huo. Alifafanua kuwa Bima ya Afya kwa Wote inalenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora, endelevu na za uhakika za afya bila vikwazo vya kifedha, jambo litakalosaidia kuongeza tija ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Dkt. Saqware aliongeza kuwa TIRA itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa bima kwa ujumla, hususan bima ya afya.

Zoezi hilo la upandaji miti limefanyika katika hali ya mshikamano, uzalendo na uwajibikaji, likionesha dhamira ya TIRA katika kuunga mkono juhudi za Serikali na kuenzi maono ya Mheshimiwa Rais ya kujenga Tanzania ya kijani, yenye afya njema na maendeleo endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.