Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
TIRA yaendesha mafunzo maalum kuimarisha uelewa wa kudhibiti udanganyifu katika bima
18 Dec, 2025
TIRA yaendesha mafunzo maalum kuimarisha uelewa wa kudhibiti udanganyifu katika bima

Katika jitihada za kuhakikisha Soko la Bima nchini linaendelea kuwa imara, endelevu na lenye ustawi, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imeendesha mafunzo maalum kwa Maafisa Madai na Maafisa Sheria wa kampuni za bima nchini. Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uelewa kuhusu hali ya udanganyifu katika bima na mbinu za kuzuia na kutokomeza vitendo hivyo.

Akifungua mafunzo hayo, Kamishna wa Bima, Dkt. Baghayo Saqware, amesema kuwa Mamlaka imebaini kuwepo kwa vitendo mbalimbali vya udanganyifu katika sekta ya bima, hali iliyosababisha kuanzishwa kwa Kitengo cha Udhibiti wa Udanganyifu kwa lengo la kudhibiti na kukomesha vitendo hivyo. Amewahimiza Maafisa Madai na Sheria kushirikiana kwa karibu na TIRA kwa kuripoti viashiria vyote vya udanganyifu ili kulinda uadilifu wa soko la bima.

Kwa upande wake, Meneja wa Kitengo cha Udhibiti wa Udanganyifu, Bw. Okoka Mgavilenzi, alimshukuru Kamishna wa Bima kwa hotuba ya ufunguzi, akibainisha kuwa ujumbe huo umetoa mwelekeo na onyo kwa wadau kuhusu msimamo thabiti wa TIRA katika mapambano dhidi ya udanganyifu katika bima. Aidha, alisisitiza kuwa Kitengo hicho kiko tayari kushirikiana na Maafisa Madai na Sheria wakati wote ili kubaini, kuchunguza na kushughulikia matukio ya udanganyifu katika sekta ya bima.

Mafunzo hayo pia yalihudhuriwa na Wachunguzi wa Masuala ya Udanganyifu wenye ithibati (Association of Certified Fraud Examiners – ACFE) wakiwakilishwa na Rais wake Bw. Ali Mabrouk. Aidha, Bw. Mabrouk ameeleza kuwa ACFE itaendelea kushirikiana na TIRA na Soko la bima katika jitihada ya kuwajengea uwezo wa wadau wa soko kwa ujumla  ili kuongeza ufanisi wa kudhibiti udanganyifu kaika soko la bima.