TIRA yaeleza TEHAMA inavyoleta ufanisi katika kutoa huduma za bima nchini

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa bima kupitia kipindi cha Kumepambazuka kinachorushwa na Radio One na kufikiwa na takribani Watanzania milioni mbili nchini kote. Katika kipindi hicho, wawakilishi kutoka TIRA walieleza namna matumizi ya TEHAMA yanavyoboresha huduma za bima na kuimarisha usalama wa soko la bima nchini.
Bw. Ali Othman, Meneja TEHAMA wa TIRA, alisema kuwa kwa sasa soko la bima linaendeshwa kidijitali kwa asilimia 100 kupitia mifumo ya kidijitali ya kisasa kama TIRAMIS na ORS. Mifumo hii inasomana na mifumo mingine ya kitaifa ikiwemo ya Jeshi la Polisi, NHIF, LATRA, TRA, NIDA na BRELA, hivyo kuwawezesha watumiaji kupata huduma za usajili na uhakiki wa bima popote walipo.
Aidha, mfumo wa TIRAMIS umewezesha ukataji na uhakiki wa bima kufanyika kidijitali, huku watumiaji wakipata fursa ya kutumia pia programu maalumu inayopatikana kwenye Google Playstore kwa simu za Android. Kupitia mfumo huu, mteja anaweza kujiridhisha endapo chombo cha usafiri kimekatiwa bima halali.
Kwa upande wake, Bw. Ayubu Mremi, Mtakwimu wa Bima, alisisitiza wajibu wa TIRA katika kulinda haki za walaji wa bima kwa kushughulikia malalamiko na changamoto mbalimbali. Pia alikumbusha kuwa ni kosa la kisheria kwa chombo chochote cha moto kutumika barabarani bila bima.
Ameeleza kuwa kufuatia kupitishwa kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote inayomgusa kila Mtanzania, TIRA imepewa jukumu kubwa la kusimamia utekelezaji wake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya afya na bima. Alisisitiza kuwa Mamlaka ina jukumu la kuhakikisha wananchi waelewe umuhimu wa kuwa na bima ya afya, hatua za kujiandikisha na namna ya kupata huduma kwa urahisi. Pia, aliweka wazi kuwa lengo la sheria hiyo ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya bila kuathiri hali yake ya kifedha, huku ikichochea usawa na mshikamano wa kijamii.
TIRA imesisitiza kuwa itaendelea kutoa elimu ya bima kupitia majukwaa mbalimbali ili Watanzania waelewe umuhimu wa bima, wajikinge na majanga yasiyotabirika na wafahamu kuwa Mamlaka ipo tayari kuwasaidia pale wanapokutana na changamoto za kibima.