TIRA yadhamini na kushiriki katika Tuzo za Ubora katika Sekta ya Mawasiliano 2025 Zanzibar

Katika usiku uliosheheni shangwe, hamasa, na utambuzi wa ubora wa mawasiliano, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) iling’ara vilivyo — si kama mgeni tu, bali kama mdhamini na mshirika muhimu wa maendeleo ya taaluma ya mawasiliano nchini na kupata tuzo maalum.
Tuzo za Ubora wa Mawasiliano (Zanzibar Communication Excellence Awards - ZACEA) zilifanyika katika ukumbi wa Golden Tulip Hotel, tarehe 7 Agosti 2025 ambapo zilikutanisha wataalamu wa mawasiliano, Taasisi za Serikali, vyombo vya habari, kampuni za Mawasiliano, pamoja na wadau kutoka sekta binafsi na za umma kutoka Visiwani humo na Bara. Mgeni Rasmi akiwa ni Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Mhe. Shariff Ali Shariff. Lengo kuu la tukio hili lilikuwa ni kutambua na kuenzi juhudi za ubunifu na ubora katika tasnia ya mawasiliano.
Waziri Mhe. Shariff alisisitiza juu ya uwajibikaji na utoaji habari zinazoelezea mambo mazuri mengi yanayofanywa na Serikali za pande zote mbili (Bara na Visiwani) na kuwataka Waandishi wa Habari na Maafisa Mawasiliano kuchagua maeneo ya ubunifu na kuwa mahiri kusemea habari zake ili wananchi waweze kupata taarifa mbalimbali.
TIRA ilishiriki kikamilifu ama mdhamini wa hafla hiyo ambapo ilithibitisha dhamira yake ya kukuza mawasiliano yenye weledi, uwazi, na ushirikishwaji katika taasisi za umma.
TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA