TIRA na DSE Wasaini Makubaliano ya Kupanua wigo Sekta ya Fedha Nchini

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) leo wameingia kwenye makubaliano rasmi ya ushirikiano wa kimkakati kwa lengo la kukuza na kupanua sekta ya fedha nchini.
Makubaliano hayo yamesainiwa jijini Dar es Salaam kati ya Kamishna wa Bima, Dkt. Baghayo Saqware, na Mkurugenzi Mtendaji wa DSE, yakilenga kushirikiana katika maeneo manne ya msingi, ikiwemo utoaji wa mafunzo, kuboresha uelewa wa umma juu ya bidhaa za kifedha, kukuza masoko ya mitaji, na kuimarisha ujumuishaji wa kifedha.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Kamishna wa Bima Dkt. Saqware alisema kuwa ushirikiano huo utafungua fursa zaidi kwa kampuni za bima nchini kuongeza mtaji wao kupitia masoko ya mitaji, ikiwemo utoaji wa hati fungani na mauzo ya hisa kwa umma.
"Masoko ya bima yana uhusiano wa karibu na masoko ya mitaji. Kwa kuunganisha nguvu, taasisi zetu zitasaidia kuwezesha kampuni za bima kutumia fursa zilizopo katika soko la hisa ili kuimarisha uwezo wao wa kifedha," alisema Dkt. Saqware.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa DSE Bwn. Peter Nalitolela, alieleza kuwa makubaliano hayo ni hatua muhimu katika kuleta mapinduzi ya kifedha nchini, hususan katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu bidhaa za bima na uwekezaji, pamoja na kuunga mkono juhudi za serikali za kuongeza ushiriki wa wananchi katika sekta rasmi za kifedha.
“Tunatarajia kuona ongezeko la uelewa kwa umma kuhusu huduma za kifedha, na kwa pamoja tutachangia katika kujenga uchumi jumuishi unaowanufaisha Watanzania wote,” alisema.
Makubaliano haya yanatajwa kuwa hatua ya kimkakati katika kufungua fursa mpya kwa taasisi za fedha nchini, kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa makundi mbalimbali ya wananchi, na kuimarisha mazingira rafiki ya uwekezaji ndani ya Tanzania.
TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA