TIRA Kanda ya Kaskazini yashiriki matembezi kuadhimisha Siku ya Wagonjwa wa Sickle Cell Arusha, elimu ya bima yatolewa

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kupitia Kanda ya Kaskazini, tarehe 10 Septemba 2025 ilishiriki matembezi maalum ya kuadhimisha Siku ya Wagonjwa wa Sickle Cell yaliyofanyika jijini Arusha, katika Hospitali ya Mount Meru.
Katika maadhimisho hayo, Afisa Bima wa TIRA Kanda ya Kaskazini, Bw. Goodluck Massawe, alipata fursa ya kutoa elimu kwa wananchi na wadau mbalimbali kuhusu umuhimu wa kuwa na bima ya afya. Alisisitiza kuwa bima ya afya ni nyenzo muhimu inayoweza kuwasaidia wananchi kuepuka gharama kubwa za matibabu, pamoja na kuhakikisha wanapata huduma bora na za uhakika.
Aidha, Bw. Massawe alieleza kuwa TIRA kwa sasa imeanza kusajili vituo vya afya vitakavyoshiriki katika mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote, kama sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote iliyopitishwa hivi karibuni. Alibainisha kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za afya kwa urahisi na kwa gharama nafuu.
Vilevile, TIRA ilitumia fursa hiyo kuufahamisha umma kuwa Hospitali ya Mount Meru tayari imesajiliwa rasmi na Mamlaka, hatua inayowezesha kituo hicho kutoa huduma chini mfumo wa bima ya afya.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya afya, watoa huduma na wananchi, ambapo pamoja na matembezi, washiriki walipata elimu kuhusu namna bora ya kujikinga na kudhibiti ugonjwa wa Sickle Cell.
TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA