Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
TIRA, FSDA wakutana kujadili ukuzaji wa sekta ya bima nchini na uchumi
05 Feb, 2025
TIRA, FSDA wakutana kujadili ukuzaji wa sekta ya bima nchini na uchumi

Februari 05, 2025

Mkutano kuhusu sekta ya bima nchini umefanyika hapo jana Februari 04, 2025, jijini Dar es salaam ukifunguliwa rasmi na Naibu Kamishna wa Bima Tanzania Bi. Khadija Said. Mkutano huo ambao uliandaliwa na FSD Africa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) umelenga kuwakutanisha wadau wa sekta hiyo kuangazia masuala ya Uchumi na bima na njia zitakazoweza kutumika na kuleta mazingira bora zaidi ya kiuchumi hasa kwa wananchi wa Tanzania na Africa kwa ujumla.

Bi. Khadija alitoa rai kwa washiriki hao kutumia jukwaa hilo kwa majadiliano yenye tija na kutafakari njia za kukuza Uchumi huku pia sekta ya bima ikijikita kutengeneza bidhaa mbalimbali zitakazoweza kudumu muda mrefu na zenye unafuu kwa wananchi, ili kila Mtanzania apate huduma za bima, akikazia zaidi upande wa afya.

Nae Bw. Elias Omondi Afisa Mkuu Ubunifu na Ustahimilivu FSD Africa, alisema taasisi hiyo imejikita katika kujenga na kuboresha mifumo mbalimbali ya fedha ili kukuza uchumi na TIRA kama kiungo muhimu katika uchumi wa nchi ina nafasi kubwa ya kuendelea kuboresha maisha ya watanzania kupitia sekta ya bima itakayoweza kuwasaidia pale wanapokubwa na majanga mbalimbali yakiwemo magonjwa.

Pia Mshauri wa Maendeleo kwa Sekta Binafsi kutoka Ubalozi wa Uingereza Tanzania, Bw. Alex Mangowi  ameipongeza Mamlaka kwa ukuaji wa sekta hiyo nchini kwa kuwepo kwa ongezeko la watoa huduma, ongezeko la ulipaji wa madai, michango ya bima katika pato la taifa, thamani ya mitaji lakini pia ubakizaji wa ada nchini na kusisitiza ubunifu, na unafuu wa bidhaa ili kuendelea kuwa na soko la bima imara.

Washiriki pia walipata nafasi ya kufanya majadiliano na mawasilisho  ambapo TIRA iliwasilishwa na Meneja wa Idara – Uendelazaji Soko Bw. Edgar Shao  kwa kuwasilisha  kuhusu  Importance of Insurance  Regulatory Sanbox pia Bw. Alex Rocky Meneja Kitengo cha Tathmini na Uchambuzi wa Takwimu  alishiriki mdahalo na kuzungumzia mambo mbalimbali yakiwemo  ushiriki wa Mamlaka katika kuunda konsotia mbalimbali kama za Kilimo, Mafuta na Gesi ambazo zinasaidia kuleta unafuu katika bima na kukuza soko.

Mkutano huo umehudhuriwa na watendaji wakuu wa kampuni za bima, Washauri wa Bima, Mawakala wa Bima, Kampuni za Bima Mtawanyo, Benki Bima na wadau wengine muhimu.

TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA