Naibu Kamishna wa Bima Azindua Rasmi Akiba Flex Plan: Suluhu Bunifu la Akiba na Ulinzi wa Maisha kwa Watanzania

Leo, tarehe 20 Mei 2025, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imeshiriki katika uzinduzi rasmi wa bidhaa mpya ya Akiba Flex Plan kutoka kampuni ya Jubilee Life Insurance, bidhaa iliyobuniwa mahsusi kuwasaidia Watanzania kuwekeza fedha zao huku wakijihakikishia ulinzi wa maisha yao. Hafla hiyo ya uzinduzi imefanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya bima, taasisi za kifedha, pamoja na wawakilishi kutoka serikalini.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Bima Tanzania, Naibu Kamishna wa Bima, Bi. Khadija Said, aliipongeza kampuni ya Jubilee Life Insurance kwa kuendelea kuonesha ubunifu unaolenga kutoa suluhu ya kweli kwa changamoto za kifedha zinazowakumba Watanzania wa makundi yote. Alisema kuwa bidhaa kama Akiba Flex Plan si tu kwamba inatoa fursa ya kujiwekea akiba, bali pia inahakikisha kuwa wananchi wanapata ulinzi wa maisha yao kupitia bima, muunganiko wa kipekee wenye manufaa makubwa kwa mtu binafsi na familia yake.
Bi. Khadija alisisitiza kuwa upatikanaji wa bidhaa jumuishi kama Akiba Flex Plan ni hatua madhubuti ya kuwawezesha wananchi kupanga maisha yao ya baadaye kwa usalama na uhakika. Aidha, alieleza kuwa Mamlaka itaendelea kusimamia upatikanaji wa huduma bora za bima kwa wote, huku ikisisitiza ulipaji wa madai kwa wakati ili kuongeza imani ya wananchi katika sekta hiyo muhimu ya uchumi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Jubilee Life Insurance, Bw. Amyn Lalji, alisema kuwa Akiba Flex Plan ni jibu la kimkakati kwa mahitaji yanayobadilika ya wateja waliopo na wale wapya. Alieleza kuwa bidhaa hiyo inaleta pamoja unafuu wa kifedha, nidhamu ya kuweka akiba, na urahisi wa matumizi ya kidijitali kwa pamoja. Alisema kuwa ili kukidhi kasi ya mabadiliko ya kiuchumi, ni muhimu kwa watoa huduma kama Jubilee kuendelea kubuni bidhaa bunifu zinazogusa mahitaji ya kweli ya jamii. Aliongeza kuwa anaamini Akiba Flex Plan itawawezesha Watanzania kufikia malengo yao ya kifedha wakiwa kinga ya bima.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Jubilee Life Insurance, Bi. Helena Mzena, alifafanua kuwa bidhaa hiyo inalenga kuziba pengo kati ya ulinzi wa kifedha na uhuru wa michango ya mteja. Alisema kuwa Akiba Flex Plan inaonesha dhamira ya Jubilee kuleta bima karibu zaidi na maisha ya Mtanzania wa kawaida. “Bima si tu bidhaa ya kifedha, bali ni ahadi ya ulinzi, utu na amani ya moyo,” alisema Bi. Helena, akiongeza kuwa bidhaa hiyo imetengenezwa mahususi kwa watu ambao hawajawahi kupata huduma rasmi za bima ya maisha, pamoja na wale ambao tayari wanatumia bima lakini wanahitaji chaguo la ziada lenye unafuu na ufanisi.
Uzinduzi huu unathibitisha kuwa sekta ya bima nchini Tanzania inaendelea kukua kwa kasi, huku bidhaa kama Akiba Flex Plan zikionesha njia mpya na bunifu za kuongeza ushiriki wa wananchi katika huduma rasmi za kifedha, kwa ajili ya ustawi wa mtu mmoja mmoja na maendeleo ya taifa kwa ujumla.