Mkutano wa Tatu wa Baraza la Nne la Watumishi wa TIRA wafanyika; watajwa chachu ustawi Sekta ya Bima

Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, na kila penye watu mshikamano ni nguzo kuu. Kauli hiyo imedhihirika katika Mkutano wa Tatu wa Baraza la Nne la Watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ambapo watumishi hao wamekutana kwa umoja wao kujadili masuala mbalimbali kwa maendeleo ya Taasisi hiyo, sekta ya bima na Taifa kwa ujumla. Mkutano huo wa siku mbili kuanzia tarehe 15 – 16 Oktoba unafanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Jengo la Ukaguzi, Dodoma.
Akisoma Hotuba yake wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo Naibu Kamishna wa Bima na Makamu Mwenyekiti wa Baraza,Bi. Khadija Said amesisitiza Baraza la wafanyakazi lina nafasi ya kipekee katika kuhakikisha uwiano kati ya Usimamizi wa Taasisi na Watumishi lakini pia malengo ya pamoja katika ufanisi wa kazi yatakayowezesha umoja kwa ustawi wa watumishi, watoa huduma za bima na wananchi kwa ujumla.
Aidha, Bi. Khadija pia alieleza TIRA imeendelea kufanya mageuzi makubwa katika utendaji wake, ikiwemo kuimarisha mifumo ya kidijitali, ongezeko la bidhaa mpya katika soko, utoaji elimu kwa umma kuhusu masuala ya bima, na kuhakikisha watoa huduma za bima wanazingatia sheria, kanuni, na viwango bora vya utoaji huduma. Na kueleza mafanikio hayo yanatokana bidii, ubunifu na ushirikiano katika kazi unaofanywa na watumishi hao.
Kwa upande mwingine, Mkutano huo umetoa fursa kwa watumishi kupewa elimu ya mtandao wa mawasiliano ya ndani, usalama katika TEHAMA, muundo wa Taasisi na elimu kuhusu afya ya akili. Watumishi pia walipata fursa ya majadiliano katika mada mbalimbali zilizowasilishwa ishara ya uwazi na ufanisi wa baraza hilo.
TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA