Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
Mchakato Bodi Wataalam Hifadhi ya Jamii, Bima Waanza
25 Aug, 2022
Mchakato Bodi Wataalam Hifadhi ya Jamii, Bima Waanza

Wataalmu wa bima kutoka taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi ,hifadhi ya jamii na watakwimu bima ikiwa ni kikao cha pili cha kujadili namna bora ya uanzishwaji wa bodi itakayosimamia taaluma za Hifadhi ya Jamii , Wataalam wa Bima na Watakwimu Bima nchini.

Hayo yameelezwa leo na Kamishna wa Bima nchini Dkt. Baghayo Saqware wakati wa ufunguzi wa mkutano huo  akisema imefika wakati sasa kuanzisha chombo hicho ili wanataaluma katika nyanja zilizotajwa wafanye kazi kwa kusimamia weledi pamoja na kutambuliwa kama zilivyo taaluma nyingine.

Dkt. Saqware amesema watu waliosomea taaluma za taaluma za hifadhi ya jamii (social protection), wataalam wa Bima (insurance experts) na watakwimu bima (insurance actuaries) wanahitajika na kufanya kazi sehemu nyingi sana hapa nchini lakini hawajawahi kuwa na chombo kama hiki ukilinganishwa na wahasibu na bodi yao NBAA, wanasheria, wahandisi na madaktari.

Kamishna amesema tangu nchi kupata uhuru zimefanyika jitihada nyingi za kuanzisha vyuo na nyenzo mbalimbali katika taaluma hizi hivyo ni vyema kuweka historia hii ya kuanzisha chombo ambacho kitasaidia kukuza taaluma hizi na kuhakikisha hakuna mtu anayefanya kazi hizi bila kuwa na taaluma husika. 

Huu ukiwa ni mchakato, mkutano wa kwanza uliweza kupokea wazo la kuanzisha chombo hicho pamoja na kupendekeza wajumbe wa kamati ambayo itafanya kazi ya kuhakikisha wadau wanahusishwa kwa kutoa michango ya kujenga bodi hiyo na kuweka mpango kazi. Baadae mapendekezo yatapelekwa Serikalini kwa hatua zaidi ili chombo hicho kiweze kuanzishwa na kufanya majukumu yake kisheria.

Mkutano huu wa pili umepokea majina ya wajumbe wa kamati ya uongozi (Steering Committee) hiyo ambao wanatoka Wizara ya Fedha na Mipango, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA).

Taasisi nyingine ni Chuo cha Bima na Hifadhi ya Jamii Afrika (ACISP),Umoja wa Watoa huduma za Bima Tanzania (ATI), Taasisi ya Bima Tanzania(IIT), Umoja wa Washauri wa Bima Tanzania (TIBA), Chama cha Wakala wa Bima Tanzania (IAAT), Chama cha Watakwimu (AST), Chama cha Wakadiriaji Hasara za Bima (ATLAS) na Umoja Benki wakala wa Bima (ABA).

Dkt. Saqware alifahamisha kuwa matarajio ya mchakato huo ni kuwa ifikapo Machi 2023 chombo hicho kiwe kimeanza kufanya kazi yake kadri sheria itakayokianzisha itakavyoelekeza.