MAONESHO YA BIASHARA YA TANZANITE: BIMA YA KILIMO NI NYENZO YA KULINDA MITAJI NA BIASHARA

Bima ya kilimo ni aina ya bima inayolenga kulinda wakulima dhidi ya hasara zinazotokana na majanga ya asili kama vile ukame, mafuriko, mvua kali,uchache wa mvua na milipuko ya magonjwa au wadudu.
Lengo kuu la bima hii ni kuwasaidia wakulima kurejesha sehemu ya mapato yao wanapokumbana na changamoto zinazoweza kuathiri mavuno na, hatimaye, mapato yao.
Kwa kuzingatia hilo Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania TIRA imeendelea kuelimisha wananchi hasa wakulima na wafanyabiashara kutumia bima ya kilimo ili kulinda mitaji yao na kuendeleza uzalishaji.
Uelimishaji huo unafanywa kwa njia mbalimbali ikiwemo ushiriki wa Mamlaka kwenye Maonesho mbalimbali. Mkoani Manyara katika Halmashauri ya Mji Babati, viwanja vya stendi ya zamani yanaendelea Maonesho ya Biashara ya Tanzanite ambapo Mamlaka inashiriki kutoa elimu kwa wananchi wa Babati na maeneo ya jirani.
TIRA kanda ya kati ni wenyeji wa Maonesho hayo ambapo leo tarehe 25 Octoba 2024, Meneja wa Kanda Bw. Frank Shangali alitoa elimu ya bima redio FM Manyara na pia kugusia zaidi bima ya kilimo ambayo ambayo ni muhimu kwa wananchi wa mkoa wa Manyara kwakuwa wanafanya kilimo cha aina mbalimbali.
Katika kujibu swali lililoulizwa na Mtangazaji wa kipindi cha Hello Africa kuhusu changamoto katika utoaji elimu ya bima hiyo alieleza changamoto zinakuwepo lakini kama Mamlaka wanazitumia kama fursa kutoa elimu ili kufanikisha malengo ya taasisi na matarajio ya Serikali katika kuhakikisha kila mwananchi anafahamu kuhusu bima na kutumia bidhaa zake.
Aliendelea kwa kusema Bima kwa sekta ya kilimo na ufugaji ni muhimu sana lakini changamoto ilikuwa kutumiwa na wakulima kutokana na gharama husika ambapo kwa kutambua hilo Mamlaka kwa kushirikiana na wadau wa bima zikiwemo kampuni za bima na Wizara walikuja na mpango kambambe wa bima za vikundi wananchi walipata unafuu wa bei ya kukata bima.
Pia alieleza katika kupenyeza elimu ya bima walitembelea maeneo kama Mbulu Mbulu wanapolima ngano, Magugu kilimo cha mpunga na pia Basutu kwa ajili ya kilimo cha mpunga.
Bima ni nyenzo inayoweza kuwazalishia uzalishaji na tija katika kilimo wanachokifanya pale wanapopatwa na majanga kama mvua zilizopitiliza au zilizo chini ya kiwango ‘ Tunawakikishia wananchi watalipwa kwasababu kwa takwimu asilimia 95 ya madai yanalipwa na asilimia 5 kunakuwa na viashiria vya udanganyifu na ikiwa kuna lalamiko mwananchi awasiliane na Mamlaka au kutembelea ofisi za kanda zilizopo katika mikoa mbalimbali, alisema Meneja Shangali akijibu swali la Mwananchi kuhusu utoaji wa fidia za bima.
TIRA kanda ya kati inahudumu mikoa ya Dodoma, Manyara na Iringa.
#TIRA KWA SOKO LA BIMA