Mafunzo ya bima Takaful: Elimu zaidi yasisitizwa pamoja na taarifa sahihi kwa wananchi

Mafunzo ya bima Takaful: Elimu zaidi yasisitizwa pamoja na taarifa sahihi kwa wananchi
Zanzibar,
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kwa kushirikiana na wadau wake ambao ni TAN – RE na ATI leo jumatatu Julai 28, 2025 wamefanikisha mafunzo rasmi yahusuyo bima ya Takaful kwa watoa huduma hiyo, katika bima visiwani humo. Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali.
Awali akitoa hotuba yake Mgeni Rasmi katika mafunzo hayo; Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Mhandisi Zena Said amepongeza uwepo wa semina hiyo na kusisitiza elimu zaidi kuendelea kutolewa ili wananchi wafahamu faida watakazoweza kuzipata kwa kujiunga, lakini pia alisisitiza umuhimu wa taarifa sahihi kwa wananchi ili waelewe misingi yake na namna inavyofanya kazi.
Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Bima, Bi. Khadija Said akitoa neno la ufunguzi katika semina hiyo aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano wake na sekta bima, lakini pia alisisitiza uwepo wa semina hizo una lengo la kuongeza uelewa juu ya masuala mbalimbali ya bima ambao utasaidia bima kuwa jumuishi (Inclusive Insurance)
Semina hiyo pia ilihusisha maswali mbalimbali kutoka kwa wadau iliyoibua mijadala yenye tija na kuelimisha kwa watoa huduma hao ambao ni kiungo muhimu katika kuhakikisha bima inamfikia kila mwananchi katika kujikinga lakini pia kuongeza pato la taifa.
TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA