Maafisa Mawasiliano Serikalini wanolewa utoaji wa taarifa kwa jamii na maendeleo sekta ya mawasiliano

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) inashiriki katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Maafisa Uhusiano na Mawasiliano Serikalini (TAGCO) 2025 unaofanyika mkoani Morogoro, ambao umewakutanisha Maafisa Mawasiliano wa Serikali kwa lengo la kubadilishana mawazo na kujadili masuala mbalimbali ya mawasiliano Serikalini.
Mkutano huu wa siku tano ulionza April 8 – 12 2024, umejikita katika kujadili mafanikio, mikakati na changamoto ya taaluma, kujifunza, kuimarisha ujuzi, kuandaa mikakati endelevu ya maendeleo ya tasnia, pamoja na kuibua mbinu mpya zitakazochochea ubunifu katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali ndani ya sekta ya mawasiliano.
TIRA imeshiriki mkutano huu ambapo maafisa mawasiliano wameshiriki na kuweza kuongeza ujuzi zaidi katika mada mbalimbali zilizowasilishwa zikiwemo namna ya kushirikisha shughuli za mawasiliano na Dira ya Taifa ya Maendeleo, Namna ya utoaji taarifa wakati wa majanga,matumizi ya mitandao ya kijigitali Serikalini zilizowasilishwa na wabobezi mbalimbali wa tasnia hiyo. Ujuzi huu utawasaidia kufikisha habari zenye tija na manufaa kwa wananchi.
Akitoa hotuba yake katika mkutano huo Mwenyekiti wa TAGCO Bw. Karim Meshack ametoa rai kwa maafisa mawasiliano kufanya kazi kwa weledi, ushirikiano na ubunifu lakini pa kuhakikisha wanatoa habari sahihi na kwa wakati sahihi kwa jamii katika kutangaza maendeleo mbalimbali yanayofanywa na Serikali.
Hii ni fursa mahsusi kwa wanataaluma wa mawasiliano kukumbushana umuhimu wa kushirikiana, kufanya kazi kwa weledi na kujituma, huku wakihakikisha kila mmoja anatoa mchango chanya katika kuiboresha sekta ya mawasiliano serikalini