Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
Kuelekea Uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa Soko la Bima 2024: Tujikumbushe Viashiria vya Utendaji wa Soko kwa mwaka 2023 kama alivyoeleza Kamishna wa Bima
07 Oct, 2025
Kuelekea Uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa Soko la Bima 2024: Tujikumbushe Viashiria vya Utendaji wa Soko kwa mwaka 2023 kama alivyoeleza Kamishna wa Bima

Wakati Tanzania ikielekea kuzindua Taarifa ya Utendaji wa Soko la Bima kwa mwaka 2024, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) inawakumbusha wananchi mambo muhimu yaliyojadiliwa wakati wa uzinduzi wa taarifa ya mwaka 2023.

Uzinduzi huo wa Taarifa ya Utendaji wa Soko la Bima kwa mwaka 2023 ulifanyika tarehe 22 Novemba 2024, katika ukumbi wa SuperDome, Masaki jijini Dar es Salaam, ukihudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya bima. Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad H. Chande.

Katika hotuba yake, Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware, alieleza kuwa taarifa ya utendaji wa mwaka 2023 ilionyesha ukuaji chanya wa soko la bima nchini kupitia viashiria mbalimbali ikiwemo:

  • Ongezeko la idadi ya watoa huduma za bima,

  • Kuongezeka kwa idadi ya wakata bima,

  • Uandikishwaji wa ada za bima na ulipaji wa madai,

  • Wastani wa matumizi ya fedha katika bima kwa mwananchi mmoja,

  • Michango ya sekta ya bima katika pato la taifa,

  • Thamani ya mitaji ya kampuni za bima, pamoja na

  • Ubakizaji wa ada za bima nchini.

Dkt. Saqware alibainisha kuwa lengo la sekta ya bima ni kuendelea kuongeza kwa wastani wa asilimia 15% kwa mwaka idadi ya Watanzania wanaotumia huduma za bima, ili kufikia lengo la asilimia 50% ifikapo mwaka 2050.

Aidha, alisisitiza kuwa mafanikio zaidi katika sekta ya bima yatatokana na uongezekaji wa uwekezaji endelevu, ushirikiano wa wadau, na matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma.

Katika hafla hiyo, kulifanyika pia mjadala mahsusi kuhusu Bima ya Afya kwa Wote, ulioshirikisha wadau mbalimbali kutoka taasisi za serikali na binafsi. Washiriki walijadili mikakati ya kufanikisha mpango huo pamoja na manufaa yake kwa Watanzania katika kuboresha upatikanaji wa huduma za matibabu.

Je mwaka huu kuna jipya gani? Kaa tayari kufatilia tutakuwa mubashara Youtube lakini pia fatilia kurasa zetu za Mitandao ya Kijamii kama Instagram tira_tz. Taarifa hii itazinduliwa jijini Dodoma katika Jengo la Makao Makuu ya TIRA - TIRA BIMA HOUSE lililopo Njedengwa sambamba na uzinduzi rasmi wa jengo hilo.

TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA