Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
Kilele cha Maonesho ya Nane Nane: Bima za Kilimo kwa Ulinzi Dhidi ya Majanga kwa Wakulima
09 Aug, 2025
Kilele cha Maonesho ya Nane Nane: Bima za Kilimo kwa Ulinzi Dhidi ya Majanga kwa Wakulima

Wakulima, wafugaji na wavuvi wameshauriwa kujiunga na bima ili kulinda uwekezaji wao dhidi ya majanga yasiyotabirika.

Akizungumza kwenye kilele cha Maonesho ya Nanenane, Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware, amesema TIRA imelenga kutoa elimu nchi nzima kuhusu bima za kilimo na afya, hususan kipindi ambacho serikali inawekeza kupitia mpango wa BBT. Kwa sasa, kampuni 15 zinatoa huduma za bima ya kilimo.

Akieleza faida ya bima kwa wakulima, Dkt. Saqware amesema kuwa tayari wapo ambao wameshanufaika na bima ya kilimo akibainisha kuwa mwaka 2023, wakulima wa tumbaku mkoani Tabora walilipwa zaidi ya shilingi bilioni Mbili kutokana na hasara walizopata, fedha zilizotokana na mfuko wa pamoja wa kampuni za bima za kilimo.

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Insurance na mwakilishi wa TAIC, Wilson Mzava, amesema umoja huo unaleta bima bora kwa bei nafuu na malipo ya haraka, huku ukipunguza mzigo wa kifedha kwa kampuni moja pale majanga yanapotokea.

Kwa upande wake, Msajili wa Migogoro ya Bima kutoka kwa Msuluhishi wa Migogoro ya Bima (TIO), Bw. Jamal Mwasha, amesema TIO inalinda maslahi ya watoa huduma na wateja wa bima kwa kutatua migogoro kwa njia mbadala, na amewataka wananchi wasisite kuwasilisha malalamiko yao ili kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.