Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
Mhe. Mha. Zena: Bodi ya Wataalam Bima, Hifadhi Jamaii, Watakwimu Bima Muhimu kwa Uchumi wa Nchi
31 Oct, 2022
Mhe. Mha. Zena: Bodi ya Wataalam Bima, Hifadhi Jamaii, Watakwimu Bima Muhimu kwa Uchumi wa Nchi

Serikali zetu zina dhamira ya kuhakikisha zinawaletea maendeleo wananchi kutokana na mageuzi makubwa yanayoendelea kuyafanywa katika sekta zote za uchumi nchini.

Hayo yalisemwa na Mhe. Mhandisi Zena A. Said Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Zanzibar mwishoni mwa wiki wakati akifungua mkutano wa tatu wa wadau kuelekea uanzishwaji wa Bodi ya Wataalam wa Bima, Hifadhi Jamii na Watakwimu Bima uliofanyika jijini Zanzibar katika Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA).

Kiongozi huyo alisema “Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa pamoja zinayo dhamira ya dhati kabisa ya kuleta maendeleo kwa wananchi kutokana na mageuzi makubwa yanayoendelea katika sekta zote za uchumi nchini”.

Serikali imekuwa ikitoa muongozo na maelekezo mbalimbali na kuweka mazingira bora ili kuwaletea wananchi maendeleo ya kiuchumi.

Akiongelea uanzishwaji wa bodi hiyo, Mhe. Zena alisema jambo hili limekuja kwa wakati kwani linaendana na jitihada za Serikali kuhakikisha uwekezaji unakuwa na tija nchini. Alifafanua kuwa “Wazo hili la uanzishwaji wa bodi ya wataalam kwenye sekta ya fedha kwetu kama Serikali tunaliona ni muhimu kwa sababu linashahabiana na malengo ya Serikali kwenye uwekezaji hasa kwa kuongeza confidence kwa wawekezaji”

Aidha, aliiagiza kamati ya wataalamu inayoshughulika na uanzishwaji wa bodi hiyo kuweka mipango na taratibu inayoakisi uhalali wa kisheria. Alisema, “Andaeni mpango madhubuti utakaowawezesha kukamilisha suala hili muhimu kwa wakati, fuateni taratibu na sheria zote ili chombo hiki kiwe na nguvu ya kisheria”

Awali, Naibu Kamishna wa Bima ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uendeshaji wa mchakato wa uanzishwaji wa bodi hiyo alimwambia Katibu Mkuu Kiongozi wa Zanzibar kuwa, bodi ikiundwa itakuwa na manufaa makubwa kwani taalum hizi zitatambulika na kuwa na mchango mzuri katika maendeleo ya uchumi ikiwa ni pamoja na kuangalia maslahi, weledi na maadili ya wanachama wake. Akasisitiza kuwa, “Wazo la kuanzishwa kwa bodi hii ya wataalam wa bima, hifadhi jamii na watakwimu ni muhimu kwa sasa kutokana na ukuaji wa sekta ya fedha nchini”

Ikiwa ni mkutano wa tatu wa kupanga na kujadili jinsi ya kuundwa kwa bodi hiyo kamati ya ufundi ilipata wasaa wa kueleza mpaka sasa mchakato umefikia wapi. Hata hivyo, kinachofuata sasa ni kufanya utafiti wa muundo wa bodi hiyo kwa kuwahusisha wanataaluma kutoka vyuo mbalimbali,  wananchi ikienda sambasamba na kujifunza kutoka bodi  nyingine kama hii inayofanyiwa kazi. Mkutano kama huu utafanyika Januari 2023 kwa ajili ya kupokea taarifa na mapendekezo ya kamati na hatimaye kuruhusu taratibu nyingine za kisheria kufuata.