Elimu ya bima yatolewa kwa wanafunzi wa udereva Mwanza; njia za kidigitali uhakiki wa bima zaelezwa

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) kupitia Ofisi ya Kanda ya Ziwa, tarehe 26 Agosti, 2025 imeendesha mafunzo maalum ya bima kwa madereva wanafunzi zaidi ya 150 wa chuo cha VETA jijini Mwanza. Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa bima, hususan kwa madereva wapya wanaoingia kwenye sekta ya usafirishaji wa abiria na mizigo.
Kupitia mafunzo hayo, wanafunzi walipatiwa elimu ya aina mbalimbali za bima sahihi za vyombo vya moto. Aidha, walifundishwa namna ya kuchagua bima stahiki kulingana na aina ya chombo cha moto na matumizi yake, jambo linalosaidia kupunguza migogoro na athari zinazoweza kujitokeza wakati wa majanga.
Mbali na hayo, TIRA pia iliwaelimisha washiriki kuhusu mchakato sahihi wa kuwasilisha madai ya bima pindi ajali au tukio la hatari linapotokea.
Vilevile, walifundishwa njia rahisi na za kidigitali za kuhakiki bima za vyombo vya moto ili kuepuka bima ghushi. Hatua hii inatarajiwa kusaidia kukuza nidhamu na uelewa wa bima miongoni mwa madereva na hivyo kuongeza usalama barabarani.