Bima ya afya kwa wote: Kwa huduma za afya bora, endelevu na za uhakika kwa watanzania
Serikali imetangaza kuanza rasmi kwa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote kuanzia tarehe 26 Januari 2026, ambapo kaya zitajiunga kwa gharama ya Shilingi 150,000 kwa mwaka kwa kaya isiyozidi watu sita (6). Wananchi wasio na uwezo, wakiwemo wazee, watoto, wajawazito na watu wenye ulemavu, wataendelea kugharamiwa na Serikali.
Akizungumza tarehe leo 23 Januari 2026 jijini Dodoma katika Kikao Kazi cha Kujadili Utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote kilichowakutanisha viongozi na watendaji wa ngazi za mikoa, wilaya na serikali za mitaa, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema mpango huo unalenga kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora, endelevu na za uhakika za afya kupitia skimu za bima ya afya zilizosajiliwa. Ameeleza kuwa gharama hiyo itamhusisha mwanachama mkuu, mwenza wake pamoja na wategemezi wanne, huku utoaji wa huduma ukizingatia utaratibu wa rufaa katika vituo vya afya vilivyoingia mikataba na skimu za bima ya afya.
Akiwasilisha mada katika kikao hicho, Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo A. Saqware, ameeleza majukumu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) katika kusimamia utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, akibainisha kuwa Mamlaka imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kimkakati ili kuhakikisha Sheria hiyo inatekelezwa kwa ufanisi. Amefafanua kuwa miongoni mwa vipaumbele vya TIRA ni utoaji wa elimu kwa umma kwa lengo la kujenga uelewa mpana kwa Watanzania na kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa nyuma katika utekelezaji wa mpango huo.
Dkt. Saqware ameongeza kuwa TIRA itaendelea kuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote kwa kuwekeza katika mifumo ya kisasa ya usimamizi wa bima, sambamba na maelekezo ya Serikali kama alivyoeleza Waziri wa Afya. Amesema lengo kuu ni kuhakikisha wateja na wanufaika wa bima wanapata huduma bora za bima kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo.
Aidha, TIRA imeandaa muongozo maalum unaoainisha utaratibu wa kupokea na kushughulikia malalamiko yanayohusiana na utoaji wa huduma za Bima ya Afya kwa Wote, kwa lengo la kutatua changamoto zitakazojitokeza na kuimarisha ulinzi wa wanachama wa bima.
Serikali imezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa, viongozi na watendaji katika ngazi zote kushirikiana kikamilifu katika kuhakikisha elimu sahihi kuhusu Bima ya Afya kwa Wote inawafikia wananchi kwa wakati, ili kufanikisha azma ya Taifa ya kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa Watanzania wote.
