WATUMISHI WA MAHAKAMA WANOLEWA ELIMU YA BIMA
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima Tanzania (TIO) leo Septemba 20, 2024 imefanya semina kwa watumishi mbalimbali wa Mahakama ya Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam. Lengo kubwa likiwa kutoa elimu ya bima.
Bw. Aderickson Njunwa ni Afisa Sheria Mwandamizi kutoka TIRA akitoa mada alianza kwa kueleza majukumu mbalimbali ya Mamlaka pamoja na kazi za Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima Tanzania. Pia alifafanua kuhusu wadau wa bima, zikiwemo kampuni za bima, wakala wa bima, wakadiria hasara, kampuni za bima mtawanyo, polisi, mahakama n.k. ambao wote wana kazi muhimu katika kuendeleza sekta ya bima nchini.
Watumishi hao pia walipewa elimu ya madai ya bima zikiwemo tofauti za Dai la bima, Lalamiko la bima na Mgogoro wa bima, hivyo kuwataka watumishi hao wa Mahakama kuwasaidia wananchi wanaoleta madai yao kwa kuwaeleza sehemu stahili ya kutatua ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania na Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima.
Zaidi pia waliombwa kuwaelimisha wahanga wa ajali za barabarani ambao wana madai katika kampuni za bima kuhakikisha wanakuwa na taarifa muhimu zikiwemo taarifa za kipolisi na nyaraka za matibabu.Lakini pia kuwaelimisha kuhusu TIRA kwa ajali ya utatuzi wa malalamiko yao.
Msuluhishi wa Migogoro ya Bima Tanzania Bi. Margaret Mngumi pia alishukuru Uongozi wa Mahakama ya Mkazi Kisutu kwa nafasi ya kutoa elimu hiyo “Natumaini kuna mambo mapya mmeyapata na sisi tupo wazi kushirikiana na nyie katika kuwatumikia wananchi, tuwasiliane wakati wowote mkiwa mnahitaji binafsi kuhusu bima au majukumu ya kuendeleza sekta ya bima nchini’’ alimaliza.
#TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA