Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
TIRA yahimiza mabenki kupunguza ujira gharama ya bima ziwe rahisi
24 Feb, 2025
TIRA yahimiza mabenki  kupunguza ujira gharama ya bima ziwe rahisi

Kamishna wa Bima, Dkt. Baghayo Saqware, amewahimiza watoa huduma za bima, hususan mabenki, kupunguza ujira wanaodai kutoka kwa kampuni za bima ili kupunguza gharama za usambazaji wa huduma hiyo. Ameyasema hayo leo, 24 Februari 2025, katika awamu ya pili ya ziara yake inayolenga kuhamasisha utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, Kanda ya Magharibi, na Kanda ya Ziwa Tanganyika, ikianza mkoani Shinyanga.

Lengo la ziara hiyo ni kuwaelimisha wakuu wa mikoa, makatibu tawala, na watumishi wa serikali kuhusu umuhimu wa bima, kutambulisha ofisi za kanda za TIRA na majukumu yake, pamoja na kuwaandaa kuwa mabalozi wa bima kwa wananchi wanaowahudumia.

Katika ziara hiyo, Dkt. Saqware, pamoja na wakurugenzi na watumishi wa TIRA, walikutana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, aliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa, CP. Salum Hamdun. Baadaye, walifanya mkutano wa kutoa elimu ya bima kwa watumishi wa mkoa, mkutano ambao ulifunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Bw. Julius Mtatiro.

Bw. Mtatiro alisisitiza kuwa Serikali inaendelea kuboresha mifumo ya bima ili kuhakikisha wananchi wengi wananufaika, akibainisha kuwa kupitia uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania imefanikiwa kuanzisha Bima ya Afya kwa Wote. Aliwataka watumishi wa umma kuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa bima.

Wakihitimisha mkutano huo, Dkt. Saqware alisisitiza kuwa kupunguza gharama za usambazaji wa bima kutawawezesha wananchi wengi kumudu huduma hizo, huku makampuni ya bima yakilipa kodi stahiki kwa serikali na kuongeza pato la taifa.

TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA