TIRA: MAWAKALA WA BIMA WAKUMBUSHWA KUFUATA SHERIA, KANUNI NA TARATIBU KUENDELEZA SOKO LA BIMA NCHINI
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kupitia kurugenzi ya Sheria leo Septemba 30, 2024 imefanya mafunzo kwa kutoa elimu ya bima kwa Chama cha Mawakala wa Bima Tanzania. Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Mirado jijini Dar es Salaam yakiwa na lengo la kufundisha na kukumbusha Sheria, Kanuni na Taratibu zinazotumika katika sekta ya bima.
Akifungua mafunzo hayo, Bw. Okoka Mvigalenzi; Meneja wa Utekelezaji Sheria na Kushughulikia Malalamiko kwa niaba ya Kamishna wa Bima Tanzania, amewataka mawakala hao tarkibani 200 waliohudhuria kuzingatia sheria mbalimbali zinazowaongoza katika ufanyaji kazi ili kuepuka adhabu elekezi pale wanapokiuka, ikiwemo kufutiwa usajili ili kulinda soko la bima nchini.
Afisa Bima Bw. Joseph Mfoi na Afisa Tehama Bw. Jumaa Seif kutoka TIRA pia walitoa elimu ya mifumo ya usajili inayotumiwa na TIRA ikiwemo mifumo ya ORS na TIRAMIS, ambapo mawakala hao walisisitizwa umuhimu wa kuzingatia viambatishi vyote vinavyotakiwa katika hatua za usajili au uhuishaji ili zoezi kukamilishwa kwa wakati.
Mawakala hao pia walipata nafasi ya kutoa maoni yao na kuuliza maswali mbalimbali yaliyojibiwa kikamilifu na maafisa. Kati ya maombi yao kwa Mamlaka ni kuongezewa idadi ya kampuni za bima wanazoweza kufanya nazo kazi kutoka kampuni moja kwa sasa ili kuongeza wigo wa biashara sokoni, ambapo hoja hiyo ilijibiwa kuwa jambo hilo litawezekana baada ya miaka mitatu tangu kuanza lakini pia litazingatia mwenendo wa kuridhisha wa Wakala wa Bima.
Pia Mwenyekiti wa Chama hicho Bw. Saye John Daudi amewataka mawakala hao kuendelea kufata sheria katika kazi zao, kutokufanya kazi kwa mazoea na kuhakikisha wanahudhuria kozi na semina mbalimbali ili kuwa na elimu sahihi kuhusu bima. Kozi hizo zinatolewa na taasisi kama IIT na vyuo kama IFM na ACISP.
Bw Okoka alimalizia kwa kuwahakikishia kwamba Kamishna wa Bima anafanyia kazi maombi yao mbalimbali na kuwataka waendelee kufata kanuni na taratibu ili kukuza na kuendeleza soko la bima
#TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA