Shamrashamra kuelekea Siku ya Wanawake Duniani: Wafanya utalii mbuga ya Wanyama Ngorongoro

Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani hapo kesho tarehe 8 machi 2025, leo Machi 7 baadhi ya wanawake kutoka taasisi za serikali na binafsi wamefanya utalii wa ndani kwa kutembelea mbuga ya wanyama ya Ngorongoro iliyopo mkoani Arusha, na baadhi ya wanawake kutoka TIRA wameshiriki katika utalii huo.
Safari ya tarkibani kilometa 170 ilianzia jijini Arusha hadi wilayani Ngorongoro katika hifadhi hiyo ambapo wanawake hao walipata fursa ya kuona mandhari za kuvutia zikiwemo ziwa, mabwawa, ndege na wanyama mbalimbali kama simba, tembo, nyati na nyumbu. Ikiwa kama kumbukumbu isiyosahaulika katika kusherehekea siku ya wanawake kwa mwaka 2025.
Aidha, siku ya wanawake duniani itafanyika mkoani Arusha katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiye mgeni rasmi. Maadhimisho hayo pia yalitanguliwa na maonesho ya bidhaa yaliyofanyika kwa siku saba ambapo Mamlaka ilishiriki kwa kutoa elimu ya bima kwa wananchi wa Arusha na maeneo ya jirani.
Siku ya wanawake duniani husherehekewa kutambua umuhimu wao katika jamii, ujumuishi katika maeneo mbalimbali ya kijamii, kiuchumi na kisiasa lakini pia utetezi wa haki zao na kutobaguliwa kwa jinsia yao. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “wanawake na wasichana 2025: tuimarishe haki, usawa na uwezeshaji”