Mali na miradi ya serikali ikatiwe bima kupunguza hasara za majanga - Kamishna wa Bima Tanzania

MALI NA MIRADI YA SERIKALI IKATIWE BIMA KUPUNGUZA HASARA ZA MAJANGA
Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware, ametoa rai kwa watumishi wa Mkoa wa Geita kuhakikisha kuwa mali na miradi mikubwa ya Serikali inakatiwa bima ili kupunguza hasara zinazoweza kutokea wakati wa majanga.
Dkt. Saqware amesema hayo leo, 28 Februari 2025, mkoani Geita katika ziara ya kutembelea mikoa mbalimbali, ikilenga kuhamasisha wakuu wa mikoa, makatibu tawala na watumishi wa umma kuhusu umuhimu wa bima. Ziara hiyo pia inalenga kuwaelimisha kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya bima, ikiwa ni pamoja na kuwa mawakala wa bima na utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.
Akifungua mkutano huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Bw. Mohamed Gombati, amewahimiza watumishi wa serikali kushiriki kikamilifu katika sekta ya bima na kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inalindwa kupitia bima. "Serikali inawekeza kiasi kikubwa cha fedha katika miradi ya maendeleo, hivyo ni muhimu miradi hii ikakingwa na bima ili kuhakikisha inapata fidia pale majanga yanapotokea," alisema Bw. Gombati.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Soko la Bima Tanzania, Bw. Christopher Mapunda, amesema kuwa TIRA ina jukumu la kuhakikisha elimu ya bima inawafikia wananchi wengi zaidi ili kupanua wigo wa matumizi ya bima nchini. "Kuna haja ya kuendelea kutoa elimu kuhusu bima ili wananchi waone umuhimu wake katika kulinda mali, maisha, uwekezaji na afya. TIRA itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha watanzania wengi zaidi wanapata uelewa wa bima na kunufaika na huduma zake," alisema Bw. Mapunda.
Ziara hii ni sehemu ya mkakati endelevu wa TIRA kuhakikisha bima inachukua nafasi kubwa katika maendeleo ya taifa kwa kulinda mali za umma na kuhakikisha wananchi wanakuwa na kinga dhidi ya majanga mbalimbali.