The United Republic of Tanzania

Tanzania Insurance Regulatory Authority

“TIRA kwa Soko Salama la Bima”
TIRA, Tume ya Kurekebisha Sheria na Wadau Washiriki Kikao Kazi Maoni Sheria ya Bima yatolewa
23 Oct, 2026
TIRA, Tume ya Kurekebisha Sheria na Wadau Washiriki Kikao Kazi Maoni Sheria ya Bima yatolewa

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) leo, tarehe 22 Oktoba 2026, imefanya kikao kazi jijini Dar es Salaam kwa lengo la kupokea maoni ya wadau kuhusu marekebisho ya Sheria ya Bima, Sura ya 395.

Kikao hicho kimewashirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya bima, wakiwemo wawakilishi wa kampuni za bima, chama cha waendesha pikipiki, mawakala wa bima pamoja na taasisi za Serikali, ambao wamepata fursa ya kutoa maoni na mapendekezo kuhusu maeneo yanayohitaji kuboreshwa katika sheria hiyo.

Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Ponziano Lukosi, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa TIRA, amewapongeza wadau kwa kushiriki katika mchakato huo na kusisitiza umuhimu wa kutoa maoni na mapendekezo kwa kina ili kuwezesha Sheria ya Bima, Sura ya 395, kuboreshwa na kutekelezeka kwa ufanisi. Aidha, aliongoza majadiliano ya wadau yaliyohusisha maswali na hoja mbalimbali kuhusu utekelezaji wa sheria hiyo, yakiwemo masuala ya bima katika usafiri wa reli na meli, pamoja na maeneo mengine yanayohitaji ufafanuzi na maboresho ya kisheria.

Kwa upande mwingine, Bi. Christina Binali, Mkuu wa Sehemu ya Mapitio ya Sheria kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria, amesema maoni yatakayokusanywa yatafanyiwa kazi na kuandaliwa katika rasimu ya taarifa itakayowasilishwa Serikalini kwa hatua zaidi.

Amesisitiza kuwa mchakato wa kupitia na kurekebisha sheria ni muhimu katika kuhakikisha sheria zinaendana na mabadiliko ya wakati, mahitaji ya wadau na mazingira ya sasa ya utekelezaji. Aidha, ameeleza kuwa mchakato huo unaendana na mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayosisitiza umuhimu wa kuboresha sheria na mifumo ya kisheria ili iweze kutekelezeka kwa ufanisi na kuendana na mahitaji ya maendeleo ya nchi.

 Naye, Bw. Mulokozi Athanas Kiyombo Mwanasheria kutoka Milembe Insurance ameipongeza TIRA kwa kikao hicho na kusisitiza kuwepo kwa vikao vingi vya aina hiyo ili wadau waweze kutoa maoni mbalimbali hasa katika Sheria ya Bima Sura 395.

TIRA, Kwa Soko Salama la Bima