The United Republic of Tanzania

Tanzania Insurance Regulatory Authority

“TIRA kwa Soko Salama la Bima”
Tupo Tayari Kutekeleza Sheria ya Bima ya Afya Kwa Wote - TIRA
23 Oct, 2026
Tupo Tayari Kutekeleza Sheria ya Bima ya Afya Kwa Wote - TIRA

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imeshiriki katika uzinduzi wa Bima ya Afya kwa Wote Awamu ya Pili, uliofanyika kitaifa mkoani Mtwara tarehe 22 Septemba 2026 ambapo mgeni rasmi ni Waziri wa Afya, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa.

Ushiriki wa TIRA katika uzinduzi huo ni sehemu ya juhudi za Mamlaka katika kutekeleza jukumu lake la kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma za bima, ikiwemo umuhimu wa bima ya afya katika kusaidia wananchi kupata huduma za matibabu na kujikinga na gharama zisizotarajiwa za matibabu.

TIRA yenye jukumu la kudhibiti na kusimamia bima ya afya kwa wote, imeahidi kusimamia stahiki za wanachama, watoa huduma na vituo vya afya katika utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote.

“Wanachama watapata haki zao, vituo vya afya watapata haki zao, watoa huduma watapata stahiki zao. Tunashukuru sana kwa kutuamini na tuko tayari kutekeleza Sheria ya Bima ua Afya kwa Wote. - Dkt. Baghayo Saqware, Kamishna wa Bima nchini Tanzania akizungumza mbele ya Mgeni Rasmi Mhe. Mohamed Mchengerwa alipotembelea banda la TIRA.

Pamoja na hayo, wananchi wamepata fursa ya kupata elimu na ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali ya bima, huku wakipatiwa uelewa kuhusu umuhimu wa kutumia huduma za bima kama nyenzo ya kujenga usalama wa kifedha na ustawi wa jamii.

Aidha, washiriki wa uzinduzi huo walipata fursa ya kujisajili katika Bima ya Afya kwa Wote kupitia banda la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), pamoja na kupata huduma za upimaji wa afya bila malipo katika banda la Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini.

Uzinduzi huo umehudhiriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na wadau, wakiwemo wabunge, viongozi wa Mkoa wa Mtwara, Mkurugenzi wa NHIF, viongozi wa dini na wengineo.

Hakika, Bima ya Afya kwa Wote ni hatua muhimu kuelekea upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wananchi.

TIRA — Kwa Soko Salama la Bima.