The United Republic of Tanzania

Tanzania Insurance Regulatory Authority

“TIRA kwa Soko Salama la Bima”
TIRA yapokea maoni ya wadau Marekebisho ya Sheria ya Bima Zanzibar
20 Oct, 2026
TIRA yapokea maoni ya wadau Marekebisho ya Sheria ya Bima Zanzibar

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), leo Oktoba 19, 2026, imefanya Kikao Kazi Unguja, Zanzibar, kwa lengo la kupokea maoni na mapendekezo ya wadau kuhusu marekebisho ya Sheria ya Bima, Sura ya 394, Toleo la 2023. Kikao hicho kimewakutanisha wawakilishi kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi pamoja na kampuni za bima zinazofanya shughuli zake Zanzibar.

Akifungua kikao hicho, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Sheria wa TIRA, Bw. Ponziano Lukosi, ameeleza kuwa maoni hayo yatachambuliwa na kuzingatiwa katika mchakato wa marekebisho ya Sheria hiyo kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa sekta ya bima na kushughulikia changamoto zinazowakabili wadau na umma kwa ujumla. Aidha, amewahimiza washiriki kutoa maoni yao kwa uwazi ili kusaidia kuboresha sheria hiyo na kuiwezesha kuendana na mahitaji ya sasa.

Katika kikao hicho, TIRA imewasilisha masuala muhimu yanayohusu Sheria ya Bima, Sura ya 394, na kutoa fursa kwa washiriki kujadili kwa kina vipengele vinavyohitaji maboresho. Washiriki pia wamepata nafasi ya kuuliza maswali, kutoa maoni na kupendekeza maeneo yanayopaswa kupewa kipaumbele katika marekebisho hayo. Vilevile, washiriki wamejaza na kujibu dodoso lililotolewa na Tume ya Marekebisho ya Sheria (LRCT) kwa ajili ya kukusanya maoni na mapendekezo yatakayosaidia mchakato huo.

Kwa upande wao, washiriki wamepongeza hatua hiyo ya TIRA ya kuwashirikisha wadau katika mchakato wa marekebisho ya sheria akiwemo Bw. Ali Juma Makame kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Zanzibar, ameipongeza TIRA kwa kuandaa kikao hicho, akieleza kuwa ni hatua inayoonesha uwazi na dhamira ya kuboresha sekta ya bima kwa kuzingatia mahitaji ya wakati uliopo.

Naye PrincePius Theodory, Meneja wa Kampuni ya Bima ya Bumaco, Zanzibar, amesema marekebisho hayo yamekuja kwa wakati muafaka, kwani yatatoa fursa ya kuiboresha sheria ili iendane na mabadiliko na mahitaji ya sasa, sambamba na kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Mchakato wa ukusanyaji wa maoni utaendelea katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha kuwa maoni na mapendekezo ya wadau yanakusanywa na kuzingatiwa kwa mujibu wa taratibu na sheria za nchi, kabla ya kukamilishwa kwa mchakato wa marekebisho hayo.

TIRA, kwa Soko Salama la Bima.