The United Republic of Tanzania

Tanzania Insurance Regulatory Authority

“TIRA kwa Soko Salama la Bima”
Kamishna wa Bima awataka wadau Kanda ya Kaskazini kuongeza ubunifu bidhaa za bima na kutumia fursa za kiuchumi  sekta ya bima
30 Oct, 2026
Kamishna wa Bima awataka wadau Kanda ya Kaskazini kuongeza ubunifu bidhaa za bima na kutumia fursa za kiuchumi  sekta ya bima

Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo A. Saqware, amewataka wadau wa sekta ya bima Kanda ya Kaskazini kuongeza ubunifu katika kuandaa bidhaa za bima zinazokidhi mahitaji ya wananchi na kutumia fursa zilizopo katika sekta mbalimbali za uchumi ili kupanua wigo wa huduma za bima nchini.

Akizungumza katika hafla ya chakula cha jioni (Gala Dinner) iliyofanyika mkoani Tanga tarehe 28 Oktoba 2026 na kuwakutanisha wadau wa sekta ya bima Kanda ya Kaskazini, Dkt. Saqware amesema soko la bima bado lina fursa nyingi ambazo hazijatumika kikamilifu, hivyo amewahimiza watoa huduma za bima kutotegemea bima za magari pekee, bali kuelekeza nguvu katika sekta za utalii, kilimo, mifugo, uvuvi, madini, biashara, viwanda na miundombinu.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuandaa bidhaa za bima zenye gharama nafuu, zinazopatikana kwa urahisi na zinazozingatia mahitaji na uwezo wa wananchi. Ameeleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza matumizi ya huduma za bima na kuchangia ukuaji wa soko la bima nchini.

Katika hafla hiyo, Kamishna wa Bima alizindua mpango wa Community-Based Insurance Kanda ya Kaskazini; unaolenga kushirikisha jamii moja kwa moja katika huduma za bima ili kuongeza uelewa, upatikanaji na matumizi ya huduma hizo, hususan kwa makundi ambayo hayajafikiwa kikamilifu.

Kwa upande mwingine, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), kupitia Kanda ya Kaskazini, imetoa tuzo kwa kampuni za bima, madalali, mawakala na taasisi zinazotoa huduma za bima kupitia benki (Bancassurance) zilizofanya vizuri katika uandikishaji wa bima. Tuzo hizo zilikabidhiwa na Meneja wa Kanda ya Kaskazini, Dkt. Emmanuel Lupilya, kwa niaba ya Kamishna wa Bima, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wa wadau hao katika kukuza soko la bima.

Katika hatua nyingine, Dkt. Lupilya alimkabidhi Kamishna wa Bima tuzo maalumu iliyoandaliwa na Kanda ya Kaskazini kwa kutambua mchango wake katika maendeleo ya sekta ya bima nchini.
Hafla hiyo pia ilitoa fursa kwa wadau wa sekta ya bima kukutana, kubadilishana uzoefu na kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika kupanua upatikanaji wa huduma za bima kwa wananchi.

TIRA, Kwa Soko Salama la Bima