The United Republic of Tanzania

Tanzania Insurance Regulatory Authority

“TIRA kwa Soko Salama la Bima”
KAMISHNA WA BIMA ASISITIZA UJUMUISHWAJI WA WANANCHI NA UPATIKANAJI WA VIFURUSHI NAFUU VYA BIMA YA AFYA KWA WOTE
04 Nov, 2026
KAMISHNA WA BIMA ASISITIZA UJUMUISHWAJI WA WANANCHI NA UPATIKANAJI WA VIFURUSHI NAFUU VYA BIMA YA AFYA KWA WOTE

Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo A. Saqware, ameshiriki katika mjadala kuhusu Kuimarisha Soko la Bima ya Afya kwa Wote kwa Kuzingatia Makundi ambayo Hayajafikiwa Kikamilifu na Huduma za Bima – (Engineering left behind universal health insurance) market uliofanyika katika Mkutano wa Kimataifa wa Sekta ya Fedha Barani Afrika (Africa Financial Summit – AFIS 2026), jijini Luanda, Angola, Novemba 3 hadi 4, 2026 na kufafanua masuala mbalimbali kuhusu ujumuishwaji wa wananchi na upatikanaji wa vifurushi nafuu katika Bima ya Afya kwa Wote (UHI) nchini.

Katika mjadala huo, Dkt. Saqware ameeleza juhudi zinazofanywa na Tanzania katika kuimarisha sekta ya bima ya afya kupitia utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote (UHI), unaolenga kupanua wigo wa huduma za bima ya afya na kuhakikisha makundi ambayo hayajafikiwa kikamilifu yanajumuishwa. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwa na vifurushi vya bima ya afya vyenye gharama nafuu vinavyoendana na uwezo wa kipato cha wananchi ili kuwawezesha kunufaika na huduma hizo.

Pia, ameeleza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wa bima, sambamba na matumizi ya teknolojia na ubunifu katika kuhakikisha huduma za bima ya afya zinawafikia wananchi wengi zaidi, hususan wenye kipato cha chini na wanaoishi maeneo ya vijijini.

Dkt. Saqware ameongeza kuwa TIRA, ikiwa na jukumu la kusimamia Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote nchini, imelenga kuendelea kujenga imani ya wananchi kupitia usimamizi wenye weledi, uwazi na ufanisi, ikiwemo kuhakikisha vifurushi vya bima ya afya vinakuwa na bei stahiki na huduma zinazokidhi mahitaji ya wananchi.

TIRA – Kwa Soko Salama la Bima