Waziri wa Fedha Mhe. Saada Mkuya Salum (pili kulia) akiwakabidhi Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi wa Bima Dkt. Raphael Chegeni na Kamishna wa Bima Bw. Israel Kamuzora 'Mkataba wa Huduma kwa Mteja'. Mkataba huu ulizinduliwa sambamba na Baraza la Wafanyaka kazi wa TIRA.

 

 

Waziri wa Fedha Mhe. Saada Mkuya Salum amezindua Baraza la Wafanyakazi wa (TIRA) huku akiwataka watendaji katika soko la bima kuongeza kasi ya utendaji wao hasa katika utoaji wa huduma kwa wahanga wa ajali za barabarani ambao wanazidi kuongezeka.

Aliwaambia Wafanyakazi wa Mamlaka kuwa wahanga wa ajali za barabarani wanahitaji huduma ya haraka ya kibima ili waweze kuona umuhimu wake. Katika kuhakikisha huduma ya bima inaimarika, Waziri wa Fedha alieleza kuwa "Wizara yangu itaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Bima kuhakikisha kuwa Sekta ya Bima inaimarika kwa manufaa ya Uchumi wa Taifa hili".

Pamoja na kuwapongeza Wafanyakazi wa TIRA kuwa na Baraza hilo, aliwaambia kuwa Baraza lina wajibu wa kuhakikisha kuwa linaishauri menejimenti vizuri kwa lengo la kuleta tija pamoja na mshikamano sahihi baina ya watumishi na mwajiri. Aliongeza kuwa kila mmoja mtumishi akitekeleza wajibu wake utakuwa ametimiza malengo ya Mamlaka. "Ni matumaini yangu kuwa kuanzia sasa mtafanyakazi kwa ukaribu zaidi ili kuleta matunda tunatoyatarajia kwani 'umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu'" alisisitiza Mheshimiwa Salum.

Tukio lililoenda sambamba na uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi lilikuwa ni kuzindua pia Mkataba wa Huduma kwa Mteja yaani 'Customer Service Charter'. Huu ni waraka mbao unaelezea jinsi TIRA itakavyomhudumia mteja kwa kutoa huduma inayotarajiwa kwa kuzingatia wakati na weledi. 

Akizindua mkataba huo Waziri wa Fedha alisema lengo la Mkataba huo ni kuwahakikishia wateja wenu kwamba huduma wanayoitegemea kutoka kwenu ni huduma bora na yenye haraka.

Awali kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi wa Bima Dkt. Raphael Chegeni alimfahamisha Waziri kuwa soko la bima linazidi kukua mwaka hadi mwaka hasa akirejea miaka miwili iliyopita  yaani 2012 na 2013.

Dkt. Chegeni alisema katika kipindi hicho jumla ya mauzo ya biashara ya bima iliongezeka kwa kiasi cha asilimia  17.0 kutoka shilingi bilioni 406.5 mwaka 2012  hadi  billioni  475.8 mwaka 2013.  Kwa upande wa rasilimali za makampuni ya bima (assets), alifafanua kuwa iliongezeka kwa kiasi cha asilimia 15.2 kutoka shilingi bilioni 450.5 mwaka 2012 hadi bilioni 518.9 mwaka  2013.