Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Steven Kebwe amewataka wafanyakazi wa Mamlaka ya Usimamzi wa Shughuli za Bima Nchini (TIRA) kuyaona majanga yanayowapata watanzania kama yao ili kuishauri serikali na wananchi namna nzuri ya kujikinga nayo.

Wito huu ameutoa alipokuwa akifungua kikao cha baraza la wafanyakazi wa Mamlaka hiyo kilichofanyika mjini Morogoro juma hili ili kupitia utekelezaji wa kazi za Mamlaka katika mwaka wa fedha 2017/2018.

Dkt. Kebwe alisema kulingana na ripoti ya mwenendo wa soko la bima nchini kwa sasa ni dhahiri kuwa juhudi za Mamlaka katika kusimamia soko zinaleta matunda.

“Ungezeko la ukuaji kwa kiwango cha asilimia saba 7% kwa sekta ya bima unaonyesha wazi kuwa Mamlaka ina wafanyakazi wenye uweledi, sasa ni vema nguvu zikaelekezwa katika kuelimisha watanzania kuhusu faida za bima” aliongeza Dkt. Kebwe.

Serikali imelenga kuhakikisha asilimia hamsini (50) ya watu wazima Tanzania wanatumia aina mbalimbali za bima ifikapo mwaka 2028 hatua ambayo itasaidia watanzania wengi kukingwa dhidi ya majanga na hivyo kuimarisha uchumi wao.

Hivyo, kutokana na lengo hili kubwa, Dr. Kebwe aliwataka wafanyakazi wa TIRA kutumia kikao cha baraza la wafanyakazi kuhakikisha wanafanya tathmini halisi na ya kina kwa yale yote yaliyopunguza kasi ya utendaji na kuja na suluhu itakayorahisisha lengo hilo kufikiwa.

Kwa upande wake, Kamishna wa Bima Tanzania na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi TIRA Dkt. Baghayo Saqware alisema Mamlaka imefanya mabadiliko mbalimbali ambayo kwa pamoja yamelenga kukuza na kujenga taswira nzuri ya soko la bima nchini.

“Tumeunda kamati mbalimbali zinazosimamia na kutoa maamuzi katika masuala ya kupitisha aina za bima katika soko, utatuzi wa masuala ya kisheria na kamati ya kutathini na kuratibu vibali vya bima mtawanyo (reinsurance)” alieleza Dkt. Saqware.

Kwa sasa, Mamlaka inafanya kila liwezekanalo katika soko la bima ili kuhakikisha watanzania wa kipato cha chini na kati wanafikiwa na huduma za bima.

Dkt. Saqware alisema kamati hizi zimekuwa na mchango mkubwa katika ufanisi wa kiutendaji kwa Mamlaka. Hivyo wafanyakazi pamoja na majukumu yao mengine wanapaswa kutumia ujuzi wao wa bima kushauri katika kamati hizi.

Wananchi wanapaswa kuendelea kuamini huduma zitolewazo na makampuni yaliyosajiliwa na Mamlaka kwani kufanya hivyo kutawasaidia kuinuia uchumi wao.