RC Kihongosi awataka watumishi wa serikali Simiyu kukinga mali na miradi ya serikali kwa bima

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Kenani Kihongosi amewataka watumishi wa umma mkoani Simiyu kutumia fursa kuwekeza kwenye Sekta ya Bima ili kuondokana na umasikini. Ameyasema hayo leo tarehe 5 Machi, 2025 wakati akifungua mafunzo ya bima kwa watumishi wa Umma Ofisini kwake.
Bw. Kihongosi amewasihi watumishi wa Umma mkoani Simiyu kutumia fursa ya elimu waliyoipata kuwa mawakala ili wajikwamue na umaskini. Aidha, ameagiza watumishi hao kuchukuia hatua ya kuzikatia bima mali na miradi ya Serikali ikiwemo majengo, magari na hata vifaa mbalimbali vya kazi ili kukinga vitu hivyo na majanga yanayoweza kutokea.
Awali, akizungumza katika mafunzo hayo Kamishna wa Bima Tanzania Dkt. Baghayo Saqware amesema mafunzo hayo yamelenga kutoa Elimu ya bima kwa Watumishi wa Umma mkoani huko kwa kuwahamasisha kuzikinga mali na miradi ya Serikali na kuwaeleza kuhusu fursa mbalimbali zilizopo kwenye Sekta ya Bima ili wawekeze kwa kuwa Mawakala wa Bima ili kuongeza wigo wa upatikanaji na usambazaji wa bima kwa ujumla.
Akiitambulisha Mamlaka katika mkutano huo, Meneja wa TIRA Kanda ya Ziwa, Bw. Richard Toyota, amesema Mkoa wa Simiyu umepewa kipaumbele kutokana na ongezeko kubwa la pato ghafi la bima, kutoka Shilingi Milioni 5 mwaka 2022 hadi Milioni 97 mwaka 2023, sawa na mara 19 ya ongezeko. Kwa sasa, mkoa huo una watoa huduma wa bima 13, wakiwemo mawakala 5, benkiwakala 5, wauzaji wa bima kidijitali 2, na kampuni 1 ya bima.
Hii ni fursa nzuri ya kupanua wigo wa huduma za bima na kuhakikisha wanasimiyu wengi zaidi wanapata uelewa kuhusu umuhimu wa bima katika maisha yao na shughuli zao za kiuchumi.
#TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA