Ziara ya Kamishna wa Bima: watumishi wa serikali Mara wahimizwa kuwekeza fursa zilizopo katika bima

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) leo imetoa elimu ya bima kwa watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na wajumbe wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Mara mafunzo yaliyofanyika katika ukumbi wa uwekezaji.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Mara, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi amewataka viongozi wa Serikali kuhakikisha mali, vifaa na magari ya serikali yanakatiwa bima ili kulinda mali za Serikali na majanga yanayoweza kutokea. “Hili suala la bima kwa mali za Serikali ni muhimu sana, majengo, magari na mali nyingine za Serikali zinapopata ajali inakuwa ni hasara kubwa kwa Serikali na mara nyingi zinakuwa hazitumiki tena” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema bima kama ya kilimo inaweza kuwasaidia wananchi wengi kuwekeza kwenye kilimo wakiwa na uhakika wa kupata mazao hata kama msimu huo kilimo kikiwa sio kizuri baada ya kukata bima ya kilimo. “Hii bima ya kilimo ni muhimu sana kwani wananchi wengi wanapata hasara kubwa baada ya kuwekeza na kupata majanga mbalimbali jambo ambalo mkulima huyo akiwa na bima linaepukika” amesema Mhe. Mtambi.
Awali, akiongoza kikao cha mafunzo ya watumishi, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Bw. Gerald Kusaya ameishukuru TIRA kwa kutoa elimu ya bima kwa watumishi na kuwataka watumishi kuchangamkia fursa hiyo na kuwekeza katika masuala ya bima. “Hii ni fursa nzuri kwa watumishi ambayo inawawezesha kuwa wateja wa bima mbalimbali zilizopo hapa nchini pamoja na kuwa wawekezaji katika sekta hii ya bima hata kama bado unaendelea na kazi yako” amesema Bwana Kusaya.
Kwa upande wake, Kamishna wa Bima Tanzania Dkt. Baghayo Saqware amewataka watumishi wa Serikali na viongozi kutoa ushirikiano kuweza kufanikisha malengo ya Serikali katika kuhakikisha asilimia 50 ya wananchi wanakuwa na bima. Dkt. Saqware amewataka viongozi wa Serikali kuhakikisha mali za Serikali zilizopo kwenye maeneo wanayoyasimamia zinawekewa kinga ya kibima ili kuiepushia Serikali hasara inayoweza kutokea inapotokea ajali ya aina yoyote ile.
Aidha, Dkt. Saqware amesema TIRA inatoa huduma ya ushauri katika masuala ya bima kwa mali na miradi ya Serikali na kuwahakikishia viongozi kuwa TIRA itatoa ushirikiano kama itaombwa ushauri kuhusiana na masuala ya bima. Dkt. Saqware amesema TIRA kwa mujibu wa sheria inayo majukumu ya kutoa leseni na kusajiri kampuni za bima, inatakiwa kufuatilia uendelevu wa bima hapa nchini, inapaswa kulinda haki za wateja wa bima pamoja na kutoa elimu ya bima kwa wananchi.