Watumishi Kigoma wahimizwa ushirikiano utoaji elimu ya bima - "Uelewa wa bima ni msingi utekelezaji bima ya afya kwa wote Dkt. Saqware

Kamishna wa Bima Tanzania na baadhi ya uongozi kutoka Mamlaka wameendelea na zoezi kwa baadhi ya mikoa ya Tanzania Bara, katika uhamasishaji wa matumizi ya bidhaa za bima huku msisitizo mkubwa ukiwa utoaji elimu ya bima ya afya kwa wote kwa wananchi mbalimbali.
Katika ziara hiyo, Kamishna wa Bima, Dkt. Baghayo Saqware, akiambatana na baadhi ya wakurugenzi na watumishi wa TIRA, alikutana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Ndugu Hassan Rugwa, kabla ya kufanya kikao na watumishi wa wilaya na mkoa.
Watumishi hao wamehimizwa kuimarisha ushirikiano katika utoaji wa elimu ya bima kwa wananchi, kuhakikisha wanakuwa mabalozi wa bima kwa jamii wanayoihudumia, na kusaidia katika urahisishaji wa upatikanaji wa huduma za bima kwa wananchi wa Kigoma.
Dkt. Saqware alisisitiza kuwa uelewa wa bima ni msingi wa mafanikio ya utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, hivyo ni muhimu kwa viongozi wa mkoa kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha wananchi kujiunga na huduma za bima kwa manufaa yao na maendeleo ya taifa.