Wahanga wa Ajali ya Moto Soko la Mashine Tatu Iringa wafidiwa na Bima

Wahanga wa ajali ya moto katika Soko la Mashine Tatu mkoani Iringa wamefidiwa kiasi cha shilingi milioni 120 na Kampuni ya Bima ya Reliance, leo Septemba 18, 2025, kufuatia tukio la moto lililotokea tarehe 12 Julai, 2025 na kuteketeza soko hilo kwa kiasi kikubwa.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kukabidhi hundi ya fidia kwa wahanga hao, Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware, alisema kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) itaendelea kusimamia na kuhakikisha kuwa kampuni zote za bima nchini zinatekeleza majukumu yao kwa uaminifu, ufanisi na kwa wakati ili kuleta manufaa kwa wanufaika wa huduma za bima.
Dkt. Saqware alitoa rai kwa watoa huduma wote wa bima kuhakikisha kuwa madai ya wateja yanalipwa kwa wakati na kwa usahihi ili kuimarisha imani ya wananchi juu ya sekta ya bima hapa nchini. Aidha, alizipongeza Kampuni ya Reliance na Benki ya NMB kwa kushirikiana kutoa fidia kwa wahanga kwa haraka na kwa uwazi.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Bima ya Reliance, Bw. Ravi Shankar, alisema kuwa kampuni yake imetimiza wajibu wake kwa kuwafidia wahanga hao kama sehemu ya dhamira ya Reliance Insurance ya kuwakinga Watanzania wanapopatwa na majanga. Alisema, "Baada ya tukio la moto katika Soko la Mashine Tatu, tulichukua hatua za haraka kwa kushirikiana na Benki ya NMB kufika moja kwa moja eneo la tukio. Tuliona ni vyema tuwafikie wateja wetu badala ya kuwasubiri waje ofisini kudai fidia. Tulikusanya taarifa zote muhimu kwa haraka na kuanza mchakato wa malipo. Hatua hii imeendelea kujenga imani na kuonesha kuwa soko la bima ni salama na linalojali walaji."
Naye Mkuu wa Idara ya Bima kutoka Benki ya NMB, Bw. Martine Massawe, alisema kuwa fidia waliyopewa wafanyabiashara hao 40 itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza makali ya hasara waliyoipata kutokana na janga hilo, na hivyo kuwawezesha kurejea katika shughuli zao za kiuchumi kwa haraka. Alisema, "NMB inatoa huduma za bima kwa wafanyabiashara wadogo kuanzia bima ya shilingi elfu kumi hadi laki tano. Kupitia huduma hizi, mfanyabiashara anaweza kupata fidia ya hadi milioni kumi kutegemeana na kiwango cha bima alichokichukua. Tumeweka viwango vinavyolingana na uwezo wa wafanyabiashara ili kila mmoja apate fursa ya kujilinda dhidi ya majanga. Pia, NMB imeboresha mifumo ya kushughulikia madai kwa haraka ili wahusika waweze kurejea kwenye shughuli zao bila kuchelewa."
Bw. Massawe aliongeza kuwa licha ya fidia waliyopewa, wahanga hao bado wana uwezo wa kupata mikopo ya kuendeleza na kukuza biashara zao kupitia huduma za kifedha zinazotolewa na NMB.